Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kilichofanyika jana Mji mdogo wa Orkesumet.
……………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka, amesema hahusiki kuwahamisha Mkuu wa wilaya au mkurugenzi ila wanaoweza kufanya hivyo ni mamlaka husika.
Ole Sendeka ameyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro.
Amesema hawezi kumuhamisha mkuu wa wilaya, mkurugenzi, katibu wa CCM au mtumishi yeyote kwani mamlaka hayo hana hivyo viongozi na watumishi hao wafanye kazi bila wasiwasi.
“Mimi huwa napiga ndogondogo tuu na endapo wakubwa wakisikiliza na wakikubali ndiyo huwa wanahamishwa ila sihusiki kuhamisha viongozi wa serikali hapa Simanjiro,” amesema.
Amesema hivi sasa wanazungumza lugha moja ya maendeleo na viongozi wote akiwemo mkuu wa wilaya hiyo Dk Suleiman Serera, mkurugenzi mtendaji Samwel Gunze, katibu wa CCM Amos Shimba.
“Wale waliokuwa wana wasiwasi kuwa watahamishwa au kutolewa kazini wameshapata waliyoyatarajia hivyo tufanyeni kazi jamani mimi sihusiki na chochote,” amesema Ole Sendeka.
Ameahidi kuwapa ushirikia wa kutosha viongozi wa serikali na watumishi wote wa halmashauri kwa lengo la kuhakikisha maendeleo ya wananchi wa eneo hilo yanapatikana.
“Kelele zote ninazopiga mahali popote iwe bungeni au wapi ni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa wilaya ya Simanjiro na siyo vinginevyo,” amesema Ole Sendeka.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Baraka Kanuga amesema mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Serera ni mtu mwenye maono ya maendeleo hivyo apewe ushirikiano.
“Hivi karibuni Dk Serera ameanzisha mfuko wa elimu wa wilaya kwa lengo la kutatua changamoto za elimu hivyo tumuunge mkono kwenye hilo,” amesema Kanunga.