Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akisisitiza jambo wakati akiongea na wadau (hawapo pichani) wa elimu kwenye kikao cha kujadili nyaraka mbalimbali zilizoandaliwa na Wizara jijini Dodoma, kwa lengo la kutoa maoni na mapendekezo
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akiangalia Kitabu alichokikuta katika darasa la mfano la elimu ya awali katika shule ya msingj Mtemi Mazengo iliyopo Jijini Dodoma wakati alipofika shuleni hapo kwenye kikao cha wadau wa elimu ya awali
Mmoja wa washiriki wa kikao cha wadau wa elimu akimuonyesha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof James Mdoe namna michezo inavyoweza kutumika kufundishia wanafunzi wa elimu wa awali
Baadhi ya wadau wakimuonyesha Naibu Katibu Prof. James Mdoe (Hayupo Pichani) namna nyimbo zinavyotumika kufundisha wanafunzi wa elimu ya awali kuhesabu
…………………………………………………….
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe amewataka Maafisa Elimu Maalum katika Halmashauri kushirikiana na Maafisa Elimu Kata na Jamii ili kuwatambua na kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum waliofikia umri wa kuanza shule wanaandikishwa.
Prof. Mdoe ametoa agizo hilo leo Januari 18, 2021 Jijini Dodoma alipokuwa akifungua Kikao cha wadau wa elimu cha kupitia nyaraka za uendeshaji na viwango vya utoaji wa Elimu ya Awali chenye lengo la kukusanya maoni ya kuboresha nyaraka hizo zilizoandaliwa na Wizara.
Naibu Katibu Mkuu huyo amesema Serikali imeboresha mazingira ya utoaji na upatikanaji elimu nchini ili kukidhi mahitaji ya ufundishaji na ujifunzaji na kuongeza fursa za elimu kwa makundi yote hivyo si vyema wazazi ama walezi wakawaficha watoto wenye mahitaji maalum.
“Watoto wote wana haki ya kupata elimu na ndio maana Serikali imeboresha mazingira ikiwa ni pamoja na kununua vifaa saidizi na vya kufundishia na kujifunzia ili kuondoa changamoto kwa wanafunzi, ni wajibu wa Maafisa Elimu kushirikisha jamii ili kuwatambua watoto waliofichwa ili wapelekwe shuleni,” amesisitiza Prof. Mdoe.
Akizungumza kuhusu kikao hicho, Prof. Mdoe amewashukuru wadau walioitikia wito wa kushiriki kikao hicho na kuwataka kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha nyaraka hizo kabla ya kutumika rasmi kwa lengo la utoaji wa elimu bora ya awali.
Naye Mratibu wa Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Hawa Suleiman amesema Wizara imeandaa nyaraka mbalimbali ikiwemo Mwongozo wa Uendeshaji na Viwango katika Elimu ya Awali, Mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji, Usimamizi na Uendeshaji wa Vituo Shikizi vya Shule, Kiongozi cha
Uendeshaji na Viwango katika Elimu ya Awali pamoja na Zana za Upimaji wa Matokeo ya Ujifunzaji kwa michezo.