********************
Na Victor Masangu, Kibaha
Kamati ya Siasa Kibaha imempongeza Mkurugenzi wa halmshauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde Kwa kusimamia vema utekelezaji wa miradi ya Maendeleo inayoendelea pamoja na kukamilika Kwa ujenzi wa Madarasa 47 yenye thamani ya million 940 maarufu kama Madarasa ya UVIKO-19 ambayo tayari yameanza kutumiwa na wanafunzi 2350 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Kwanza kuanzia Januari 17,2022.
Kamati hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Bundala Maulidi imeridhishwa na miradi yote minne iliyotembelewa yenye thamani ya shilingi 379,027,000 na kwamba utekelezaji wake umekwenda sanjali na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi iliyoweka Serikali madarakani inayoongozwa na Mhe.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Kamati hiyo ilianza na mradi wa ujenzi wa chumba kimoja cha darasa na msingi wa vyumba vitatu kwenye shule mpya ya Sofu ambayo tayari imeshatumia kiasi cha shilingi 22,027,000/-wananchi wakiwa wamechangia 2,027,000/- na tofali 700 wakiwa na lengo la kuwaondolea umbali mrefu wazaidi ya kilomita 8 wanaokabiliana nao wanafunzi wanapokwenda shule ya sekondari ya picha ya ndege au Nyumbu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ambaye pia ni diwani wa kata ya Sofu Mhe.Mussa Ndomba ameihakikishia kamati ya Siasa kuwa ifikapo mwezi Machi Madarasa hayo yatakuwa yamekamilika na kuanza kutumika kwani Halmashauri inatarajia kupeleka fedha kiasi cha milioni 40 Kwa ajili ya ukamilishaji ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya vyoo.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri aliishukuru kamati ya Siasa Kwa kutembelea miradi hiyo na kuahidi kuwa changamoto kidogo zilizoonekana na ukosefu wa maji kwenye shule za sekondari na upungufu wa matundu ya vyoo zitafanyiwa kazi ili wanafunzi wapate elimu kwenye maeneo bora.
Miradi iliyotembelewa ni Ujenzi wa shule ya sekondari Sofu uliogharimu kiasi cha 22,027,000 Madarasa 8 yenye thamani ya shilingi 160,000,000)- na ununuzi wa madawati shule ya msingi Maendeleo yaliyogharimu kiasi cha shilingi 2,000,000./-