***************
Na Maandshi Wetu
TAASISI ya Tanzania Peace Foundation imetoa salamu za mwaka mpya wa 2022 kwa Watanzania wote huku ikitumia nafasi hiyo kueleza hatua kwa hatua kazi kubwa ambayo inafanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Sadiki Godigodi amesema tangu mwaka mpya wa 2022 uingie hawajatoa salamu za mwaka mpya,hivyo leo wameona ni wakati sahihi wa kutoa salamu hizo na kubwa wanazungumza wakiwa na furaha kutokana kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kusimamia maendeleo.
“Tunatoa salamu za mwaka mpya kwa Watanzania wote, tunatoa salamu za mwaka mpya kwa Serikali ya Jamahuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan .Tunakiri Rais Samia ameonesha Mwanga wa matumaini katika kusimamia miradi ya maendeleo,amekuwa mbunifu katika kuleta miradi inayogusa maisha ya Watanzania
“Kwa mfano katika Mkoa wa Dar es Salaam Rais ameeleza wazi dhamira yake njema ya kuendelea kuboresha miundombinu katika sekta zote,katika barabara ameeleza wazi kuendelea kuongeza fedha za ujanzi wa barabara zikiwemo zile za mitaa,kata na wilaya za Mkoa Dar es Salaam.
“Ieleweke kwamba baada ya Rais kuingia madarakani alikuta kuna bajeti ya Sh bilioni 19 za miradi ya maendeleo ya Barabara chini ya TARURA Mkoa wa Dar es Salaam lakini aliongeza bajeti hiyo kutoka Sh.bilioni 19 hadi Sh.bilioni 44 ikiwa ni ongezeko la Sh.bilioni 25 ambalo ni zaidi ya bajeti iliyokuwepo awali,”amesema.
Ameongeza ifahamike kuwa mtandao wa barabara Mkoa wa Dar es Salaam ni kilometa 5125 ambapo nusu ya barabara hizo tayari zimeboreshwa, na nusu bado ipo katika hali ambayo si nzuri,hivyo ni vema wananchi wawe na ufahamu wa kutunza miundombinu hiyo ambayo imegharimu fedha nyinyi katika kuiboresha.
“Kuna kila sababu za kuupongeza kwa dhati kabisa uongozi wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam kwa kumuwakilisha ipasavyo Mheshimiwa Rais katika eneo la miundombinu ya barabara katika Mkoa huu.Tunatoa rai kwa taasisi nyingine kuiga mfano wa TARURA katika kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo ya Serikali ,mfano wanaohusika na miradi ya maji,afya,elimu, viwanda, nishati na aina nyingine ya miradi ya maendeleo,ni wajibu wa kila mmoja kuwajibika isavyo katika kutekeleza majukumu yao, na hapo watatimiza dhamira ya Serikali,”amesema Godigodi.
Awali kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti huyo,Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kimataifa wa Taasisi hiyo Mosses Ntandu alianza kwa kumpongeza Rais Samia kwa msimamo wake katika kuleta maendeleo ya Watanzania na kusisitiza ni vema kila mmoja wetu akasimama na Rais kwani ndiye atakayetuvusha katika kipindi cha awamu ya Sita.
“Kwa bahati mbaya kumetokea wimbi la watu kwa dhamira zao binafsi wameanza kuingiza siasa kwenye shughuli za maendeleo jambo ambalo si sahihi na Watanzania wasiingizwe kwenye ajenda hiyo maana lengo lake sio jema.Kwa kipindi kifupi sana Rais amefanya mambo makubwa mno ya kimaendeleo katika Mkoa wa Dar es Salaam ambapo pamoja na kuongoeza fedha katika bajeti ya miundombinu bado ameahidi kuongeza tena katika bajeti inayokuja,”amesisitiza.
Mkurugenzi huyo wa Mahusiano ya Kimataifa amesema kama taasii huru ni lazima wahakikishe wanamlinda Rais Samia kwa gharama zozote zile na wanaomba wananchi wote kuung mkono juhudi za Rais na yeyote ambaye ataanza kuingiza chochoko za kisiasa kwa maslahi yake binafsi ahesabiwe kuwa aduni namba moja wa Taifa na maendeleo ya Watanzania .
Ameongeza Taasisi ya Urais inapaswa kuheshimiwa na kulindwa na Watanzania wote ,hivyo wasikubali kuyumbishwa au kutolewa kwenye ajenda ya maendeleo yao wenyewe.”Hivi karibuni Rais amekuwa akihangaika huko Duniani kuhakikisha nchi inakuwa imara ndani na nje ya nchi na mpaka sasa ametuheshimisha katika mahusiano ya Kimataifa.”
Amesema hivyo katika salamu za mwaka mpya wa 2022, ujumbe wao mkubwa ni kwamba wanasimama na Mama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika miradi yote ya maendeleo, amani na usalama wa Watanzania .
Hivyo tuiheshimu, tuilinde na tuiendeleze miradi yote ya maendeleo kwa mustakabali mwema wa Taifa, tunafurahi kuona TARURA Mkoa wa Dar es Salaam wamesimama imara katika hilo.
Mwisho