………………………………………………………….
Adeladius Makwega,Moshi
Sayansi jadia ambayo inahusiana na uandaaji wa vyakula mbalimbali vya asili, uchakataji, uhifadhi, utumiaji na umuhimu wa vyakula hivyo ni mojawapo wa mambo yatakayooneshwa katika Tamasha la Kilimanjaro litakalofanyika Januari 22, 2022 Mjini Moshi.
“Vyakula hivyo vitakuwa vya jamii ya Wachaga, Wapare na Wamasai ambao ndiyo makabila yanayopatikana katika mkoa wa Kilimanjaro. Vyakula hivyo vimesaidia mno jamii zetu kwa muda mrefu kuepukana na magonjwa yanayosababishwa na ulaji hovyo wa baadhi ya vyakula.” Alisisitiza Dkt Emanuel Temu ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini.
Kwa upande wake Ombeni Mbesere ambaye ni Afisa Utamaduni alisema kuwa nia ya matamasha haya ni kuionesha jamii ya Kitanzania maisha ya wazee wetu yalivyokuwa na kuendeleza utamaduni huo kuwa urithi kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.
“Vyakula hivi ni mojawapo wa urithi tuliona ambao unaonesha namna maisha ya makabila yetu yalivyokuwa kwa miaka mingi na jambo hili ni lazima lifahamike na wengi na siyo kundi la watu wachache.” Alisisitiza ndugu Mbesere.
Mkurugenzi huyo wa utamaduni nchini akiwa ameambata na maafisa utamaduni na maafisa kadhaa wa wizara hii ameiomba jamii ya wakaazi wa Moshi wajitokeze kwa wingi kuipamba siku hiyo.
Tamasha hili la Utamaduni la Kilimajaro linafanyika kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais Wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alilolitoa huko Mwanza mwaka jana.