Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi Viti Mwendo na Kadi za Bima ya Afya kwa Watu wenye Ulemavu iliyofanyika katika ukumbi wa Boabab Ballroom hoteli ya Gran Melia, Jijini Arusha Januari 16, 2022.
Sehemu ya washiriki wakisikiliza maelezo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (hayupo pichani) wakati wa hafla ya kukabidhi Viti Mwendo na Kadi za Bima ya Afya kwa Watu wenye Ulemavu iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akisukuma kiti mwendo alichokabidhi kwa mtoto mwenye ulemavu wakati wa hafla ya kukabidhi Viti Mwendo na Kadi za Bima ya Afya kwa Watu wenye Ulemavu iliyofanyika katika ukumbi wa Boabab Ballroom hoteli ya Gran Melia, Jijini Arusha Januari 16, 2022. Wa pili kutoka kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akikabidhi kadi ya Bima ya Afya kwa mzazi mwenye mtoto aliye na Ulemavu wakati wa hafla hiyo ya kukabidhi Viti Mwendo na Kadi za Bima ya Afya kwa Watu wenye Ulemavu iliyofanyika katika ukumbi wa Boabab Ballroom hoteli ya Gran Melia, Jijini Arusha Januari 16, 2022.
Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo akieleza jambo wakati wa hafla hiyo.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi akieleza jambo wakati wa hafla hiyo ya kukabidhi Viti Mwendo na Kadi za Bima ya Afya kwa Watu wenye Ulemavu iliyofanyika katika ukumbi wa Boabab Ballroom hoteli ya Gran Melia, Jijini Arusha Januari 16, 2022.
(PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
**************************
Na: Mwandishi Wetu – Arusha
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amehamasisha wadau kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwezesha Watu wenye Ulemavu kupata vifaa saidizi na nyenzo bora za kujimudu.
Waziri Ndalichako ameyasema hayo Januari 16, 2022 katika hafla ya kukabidhi Viti Mwendo na Kadi za Bima ya Afya kwa Watu wenye Ulemavu iliyofanyika katika ukumbi wa Boabab Ballroom hoteli ya Gran Melia, Jijini Arusha.
Alisema kuwa Watu Wenye Ulemavu wanahitaji vifaa saidizi ili waweze kumudu mazingira yanayowazunguka, nyenzo hizo za kujimudu ni pamoja na viti mwendo, shime, sikio, fimbo nyeupe, ubao wa kuandikia maandishi ya nukta nundu, kofia, miwani, magongo ya kutembelea na vingine vingi, hivyo kutokana na umuhimu wa vifaa hivi upatikanaji wake ni vyema wadau wakashirikiana na Serikali katika kuwezesha Watu wenye Ulemavu kupata vifaa saidizi na nyenzo bora za kujimudu.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeweka mkazo mkubwa kwenye kuwasaidia Watu Wenye Ulemavu ikiwemo huduma za kijamii kuboresha ili kutoa fursa Watu Wenye Ulemavu kuzipata kwa urahisi,” alieleza Waziri Ndalichako
“Mmeshuhudia namna Serikali imekuwa ikikaribisha na kupokea misaada kutoka kwa wadau wa maendeleo kama hii leo walivyofanya wadau kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mrisho Gambo Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini katika kusaidia Watu Wenye Ulemavu,” alisema
Alieleza kuwa, Serikali katika kutambua uhitaji mkubwa wa vifaa saidizi kwa Watu Wenye Ulemavu Serikali imeweka jitihada ya kuhakikisha vifaa hivyo vinapatikana kwa wingi zaidi hapa nchini kwa kuanza kuzalisha vifaa hivyo kupitia Shirika la Maendeleo la Viwanda vidogodogo (SIDO). Pia, Serikali imeondoa kodi kwenye malighafi zote za kutengenezea vifaa vya Watu Wenye Ulemavu hapa nchini ili kuongeza uingizaji wa vifaa hivyo nchini na kuhakikisha vinapatikana kwa gharama nafuu.
Vile vile, alisema kuwa Serikali imeendelea kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo Watu Wenye Ulemavu katika kutafuta fursa na huduma za kijamii ikiwemo Elimu, Afya na Ajira.
Alieleza kuwa, Serikali inatekeleza Mpango wa Utoaji Elimu Bure ambao Watu Wenye Ulemavu ambao pia wanafaidika nao na katika utoaji wa Mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu, kipaumbele cha kwanza huwa ni wanafunzi wenye Ulemavu.
Pia, Waziri Ndalichako alieleza kuwa katika kipindi cha miezi tisa tangu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aingie madarakani amewezesha ujenzi wa vituo vya Afya 233, huku hospitali zikiendelea kuboreshwa na kutekeleza maagizo kuwa Watu wenye Ulemavu wasio na uwezo watibiwe bure.
Aidha alisema kuwa, Serikali imeridhia na inaendelea kutekeleza Mikataba mbalimbali ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa na kuandaa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kuwa Watu wenye Ulemavu wanapata haki zao.
Katika hatua nyingine, Waziri Ndalichako alielezea juhudi kubwa za Serikali katika uratibu na usimamizi wa utoaji wa mafunzo ya stadi za kazi na huduma za marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu kupitia Vyuo maalum vya Watu wenye Ulemavu.
“Awali kulikuwa na vyuo viwili tu vinavyofanya kazi (Chuo cha Watu Wenye Ulemavu cha Sabasaba Singida na cha Yombo-Dar es Salaam), lakini katika muda mfupi Serikali ya awamu ya sita chini ya Mama yetu Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amehakikikisha anafufua vyuo vingine kupitia fedha za UVIKO-19 kwa kutengea shilingi Billioni 8 kwa ajili ya kukarabati vyuo 5 vya watu Wenye Ulemavu,” alieleza
Aidha, alisema kuwa Vyuo hivyo vya Ufundi Stadi na marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu vimekuwa vikitoa mafunzo katika fani mbalimbali na lengo ni kuhakikisha kuwa watu Wenye Ulemavu wanapata fursa ya kupata ujuzi ambao utawasaidia kufanya kazi zitakazowawezesha kumudu Maisha yao, kuwainua kiuchumi na kuwatoa kwenye hali ya kuwa tegemezi.
Kwa Upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi alisema kuwa, Serikali imeweka Mfumo wa kuhakikisha kuwa Watu Wenye Ulemavu wanajikwamua kwenye umasikini na utegemezi ambapo Halmashauri zote nchini ziliagizwa kutenga asilimia mbili ya mapato ya ndani ya Halmashauri kutoa kama mkopo usio na riba kwa Watu Wenye Ulemavu ili kuwawezesha kiuchumi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Said Mtanda alitumia fursa hiyo kuhimiza jamii kuendelea kuwajali watu Wenye Ulemavu na kutowabagua kutokana na Ulemavu walionao.
Awali akizungumza Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mhe. Mrisho Gambo alisema kuwa Ofisi yake kwa kutambua mchango wa Watu wenye Ulemavu walionao katika jamii, wamekuwa wakishirikiana na Serikali na wadau katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazolikabili kundi hilo ili kuimarisha ustawi wao.
“Katika jimbo hili Watu wenye Ulemavu ni 1009, kati yao 440 ni wanawake na 569 ni wanaume na wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo ofisi yetu iliona umuhimu wa kutambua changamoto zinazowakabili na kutafuta njia ya kutatua na kuwa sehemu ya kufariji kundi hilo,” alisema Mbunge huyo