Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Grace Ntungi akitoa ufafanuzi kuhusu gharama za kuunganisha huduma ya umeme kwa wananchi mkoa wa Shinyanga leo Jumatatu Januari 17,2021.
**************************
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga limetangaza kuanza kutekeleza Mpango Mkakati wa kuwaunganishia umeme wananchi 3200 waliokuwa wamelipia shilingi 27,000/= mwezi Septemba mwaka 2021 kwa ajili ya kuunganishiwa huduma ya umeme huku likisisitiza gharama halisi za kuunganishiwa umeme zitafanyika kwenye maeneo ya miji na maeneo yote ya vijiji yatalipia shilingi 27,000/=.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Grace Ntungi leo Jumatatu Januari 17,2021 wakati akitoa ufafanuzi kuhusu gharama za kuunganisha huduma ya umeme kwa wananchi mkoa wa Shinyanga.
Mhandisi Ntungi amesema mpango huo wa kuwaungishia umeme wananchi hao ambao walikuwa wamelipia Shilingi 27,000/= unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 31, Machi 2022.
Mhandisi Ntungi ameeleza kuwa zoezi la kuwaunganishia huduma ya umeme wananchi wa maeneo ya Miji na Vijiji waliokuwa wamelipia shilingi 27,000 mwezi Septemba 2021 lilikwama kwa baadhi ya maeneo kutokana na changamoto ya upatikanaji wa vifaa.
“Kuna wateja ambao mwezi Septemba mwaka 2021 walilipia shilingi 27,000/= na walipewa Namba za Malipo (Control Number) na mpaka kufikia Januari 16,2022 walikuwa takribani 3200 mkoani Shinyanga walikuwa wameshafanya malipo, hivyo tutawaunganishia huduma ya umeme katika mpango mkakati wetu unaotarajiwa kukamilika ifikapo Machi 31,2022. Mpango huu hautawahusu wale waliofanyiwa Survey ambao hawakupewa Control Number”,amesema Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga.
Akielezea kuhusu bei mpya za kuunganishia umeme amesema kuanzia Januari 5,2022 ofisi ya TANESCO imeanza kutumia bei mpya za kuunganisha umeme na kwamba shilingi 27,000/= haijaondolewa kwenye maeneo yote bali itatumika kwenye vijiji vyote.
“Vijiji vyote vitalipia shilingi 27,000/=, vijiji vyote vilivyopo katika Manispaa ya Kahama na Manispaa ya Shinyanga vitalipia shilingi 27,000/= na mitaa yote italipia gharama halisi za kuunganisha umeme.
“Maeneo ya miji midogo itakayolipia gharama halisi za kuunganisha umeme ni Iselamagazi,Salawe na Tinde katika Wilaya ya Shinyanga, Nyamilangano,Lunguya na Chela wilayani Kahama na Kishapu(Mhunze) wilayani Kishapu”,ameongeza Mhandisi Ntungi.
Mhandisi Ntungi amesema maeneo yatakayolipia gharama halisi za kuunganisha umeme kwa umeme wa njia moja yaliyo ndani ya miji na Manispaa gharama ni shilingi 272,000 kwa eneo ndani ya mita 30 (bila VAT na VAT ikiongezwa jumla ni shilingi 320,960/=), eneo ndani ya mita 70 shilingi 436,964/= bila VAT na eneo ndani ya mita 120 ni shilingi 590,398/= bila VAT.
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Grace Ntungi akitoa ufafanuzi kuhusu gharama za kuunganisha huduma ya umeme kwa wananchi mkoa wa Shinyanga leo Jumatatu Januari 17,2021. Picha na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Grace Ntungi akitoa ufafanuzi kuhusu gharama za kuunganisha huduma ya umeme kwa wananchi mkoa wa Shinyanga leo Jumatatu Januari 17,2021.