Ofisa mipango wa halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Heri Kuria akisoma rasimu ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.
***********************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wamepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya sh25.2 bilioni kwa ajili ya mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Ofisa mipango wa halmashauri ya wilaya hiyo, Heri Kuria amesoma mpango huo wa bajeti kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo.
Kuria amesema bajeti hiyo imelenga kunufaisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya elimu, afya, maji na miundombinu.
Amesema katika bajeti ya 2022/2023 halmashauri hiyo itaongeza ujenzi wa madarasa ya shule za msingi 20 badala ya 15 kwano kuna upungufu wa madarasa.
Amesema wametenga sh400 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Loiborsiret na sh600 milioni za ujenzi wa madarasa ya shule mpya ya sekondari Edonyongijape.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amesema wanajitahidi kuhakikisha kata zote 18 zinapatiwa miradi ya maendeleo.
Kanunga amesema lengo ni kuhakikisha kata zote 18 zinanufaika bila kuwa na upendeleo na kufikiwa na miradi ya maendeleo.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka amesema lengo la kuhakikisha kata zote 18 zinakuwa na sekondari limefikiwa baada ya kata tatu zilizokosa nazo kujengewa.
“Kata ya Langai, Edonyongijape na Kitwai ambazo hazikuwa na shule za sekondari hapo awali hivi sasa zimepata shule za sekondari na wanafunzi watasoma,” amesema Ole Sendeka.
Diwani wa kata ya Terrat Jackson Ole Materi amesema anapongeza bajeti hiyo kwani itasaidia ujenzi wa kituo kipya cha afya kwenye eneo hilo.
Diwani wa Kata ya Loiborsiret, Ezekiel Lesenga Mardadi amesema bajeti hiyo itanufaisha wananchi wa Simanjiro hususani Kata yake kupitia kituo cha afya na elimu.
Diwani wa Kata ya Edonyongijape Jacob Kimeso amesema kwa namna moja au nyingine bajeti hiyo itachochea maendeleo ya eneo hilo hasa kwenye sekta ya elimu.