…………………………………………………………..
NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza
TAASISI ya The Desk & Chair Foundation,imetoa msaada wa madaftari wenye thamani ya sh. milioni 10 kwa wanafunzi zaidi ya 700 wanaoishi kwenye mazingira hatarishi na kuishauri Wizara ya Elimu iangalie namna ya kuwapunguzia wazazi mzigo wa gharama za kununua sare,viatu na mahitaji mengine ya shule.
Msaada na ushauri huo umetolewa leo na mwenyekiti wa taasisi hiyo,Alhaji Sibtain Meghjee,baada ya kuguswa na ukubwa wa tatizo la wazazi wengi kushindwa kumudu gharama za kununua mahitaji ya shule kwa ajili ya watoto wao.
Amesema madaftari hayo 10,998 yaliyotolewa kwa wanafunzi 720 wa shule za msingi na sekondari jijini Mwanza,yatasaidia familia zisizo na uwezo wa kuwapunguzia gharama za mahitaji ya shule kama madaftari na kupunguza mzigo wa ukubwa wa tatizo. hilo kwa baadhi ya wana jamii.
Meghjee amesema tatizo hilo ni kubwa kutokana na ongezeko la watoto wanaozaliwa na kuandikishwa shule kila mwaka ambao huungana na waliokwisha kuanza shule,hivyo taasisi hiyo iliona itoe kinachoezekana ili kupunguza changamoto hiyo kwa jamii.
“Tunaipongeza serikali kwa jitihada za ujenzi wa madarasa na kutengeneza madawati kwa shule za sekondari,imewapunguzia wazazi mzigo wa kugharamia elimu hata wasio na uwezo watawapeleka watoto shule wasome,”amesema.
Amezishangaa baadhi ya shule za sekondari mwaka huu kuwaagiza watoto kwenda na leam mbili za karatasi badala ya moja,vifaa mbalimbali ikiwemo makwanja,mifagio,ndoo na majembe ambavyo hugharimu zaidi ya sh.200,000 kwa mtoto hivyo kuwawia vigumu wazazi wote kumudu gharama.
Taasisi hiyo imekuwa ikisaidia jamii katika masuala ya afya,elimu na maji mwaka jana ilitoa msaada wa madaftari yenye thamani ya sh. milioni 9,sare na viatu vya sh. milioni 3,misaada ambayo imetoa kwa miaka mitano na mwaka huu sare na viatu vitatolewa baada ya kupata fedha kutoka kwa wafadhili.
Aidha wanafunzi akiwemo mwenye ualibinizimu Pendo Dorothei na Emmy Benjamin kwa niaba ya wenzao wamesema vifaa walivyowezeshwa vimewapunguzia wazazi gharama,vitawaongezea ari ya kujifunza kwa bidii na uandikaji wa notisi huku Emmy mwenye ndoto za udaktari wa binadamu akiahidi kufaulu mitihani yake ili kufikia malengo aliyojiwekea.
Baadhi ya wazazi wa wanafunzi walionufaika na msaada huo Mariamu Nassoro, Madua Katumba na Prisca Lucas,kwa nyakati tofauti wameishukuru taasisi hiyo kwa namna inavyowasaidia watoto wa Watanzania masikini vifaa vya shule wapate elimu na kuomba iendelee kusaidia jamii yenye uhitaji.