Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Abasi Kilima, hivi karibuni amekutana kwa mara ya kwanza na Wawakilishi wa Taasisi za Misaada ya Kijamii zenye makao yake nchini Oman ambazo zinatoa huduma za kijamii nchini Tanzania.
Katika hotuba ya kuwakaribisha Wawakilishi hao, Mhe. Balozi alisema Taasisi hizo zina mchango mkubwa kwa maendeleo ya jamii ya Watanzania na kuwataka waendelee na huduma zao hizo. Vilevile, alizitaka Taasisi hizo kutoa taarifa za miradi ya kijamii wanayoitekeleza nchini Tanzania ili mchango wao uweze kutambulika rasmi Serikalini kwani alisema ingawa mchango wao ni mkubwa kwa taifa lakini Taasisi hizo haziwasilishi rasmi taarifa zao.
Akitaja baadhi ya huduma zinazotolewa na Taasisi hizo alisema zipo Taasisi zinazochimba visima na hivyo zimekuwa zikisaidia kampeni ya Serikali ya “Kumtua ndoo mama”. Vilevile, zipo Taasisi zinazotoa huduma za elimu, kusaidia yatima, kujenga nyumba za makazi na nyumba za ibada. Aliendelea kusema kuwa, kwa kuwa viongozi wa Taasisi hizo wana asili ya Tanzania na bado wana mafungamano makubwa na nchi yao ya asili, Serikali inawatambua kama Diaspora na hivyo uwasilishaji wa taarifa za huduma wanazozitoa utasaidia lengo la Serikali la kuwapa hadhi maalum.
Mhe. Balozi Kilima alizitaka Jumuiya hizo kuwa kitu kimoja na kukutana mara moja au mbili kila mwaka kujadili masuala yao. Miongoni mwa Taasisi alizokutana nazo ni pamoja na Alwadood International, Istiqama International, Attaqwa, Tuelekezane Peponi, Sundus, Coco Charity na Alfirdaus. Pia alitumia fursa hiyo kuzipa tuzo maalum Taasisi mbili zilizofanya vizuri nchini Tanzania. Taasisi hizo ni Tuelekezane Peponi na Attaqwa. Taasisi nyengine zilizofanya vizuri zilipewa Tuzo wakati wa Sherehe za Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Katika mkutano huo, Wawakilishi wa Taasisi hizo walipata fursa ya kuelezea changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo ushuru kwa bidhaa na vifaa wanavyoleta nchini kwa ajili ya Misaada na kuiomba Serikali iwaondolee ushuru kwa bidhaa hizo. Kadhalika, walieleza changamoto nyengine ya kuchelewa kupata usajili kwa baadhi ya Taasisi, upatikanaji wa vibali na tozo za viza. Pia, wameomba Serikali iwapatie utambulisho maalum ili waweze kuingia nchini mara kwa mara kutekeleza miradi ya Kijamii.
Akitoa ufafanuzi wa changamoto hizo, Mhe. Balozi Kilima alisema ni vyema Taasisi hizo ziwasiliane na Ubalozini pale zinapohitaji kupeleka misaada ya kijamii ili Ubalozi uweze kuwatambulisha rasmi katika Mamlaka za Serikalini. Aidha, kuhusu viza aliwashauri kuomba viza ya kuingia mara kwa mara (Multiple entry visa) au viza ya kutembelea jamaa (family visit visa).
Pamoja na majibu hayo, alisema Serikali inaendelea na mchakato wa kuandaa mpango maalum wa kuwatambua Diaspora na kuwapatia hadhi maalum itakayowarahisishia utekelezaji wa shughuli zao za kijamii nchini.
Taasisi hizo kwa pamoja zimechimba visima virefu 200, visima vifupi 5000, zimejenga nyumba za yatima 17, Madrasa 62, na Misikiti 47. Aidha, Taasisi ya Alwadood inakusudia kuleta nchini mtambo wa kuchimbia visima virefu wenye thamani ya USD 170,000.