……………………………………….
Na.Alex Sonna
VINARA wa Ligi Kuu ya NBC Timu ya Yanga hatimaye imevunja mwiko wa kutokupata matokeo katika uwanja wa Mkwakwani Tanga baada ya kuwachapa wenyeji Coastal Union mabao 2-0.
Mshambuliaji hatari kwa sasa Fiston Mayele aliwanyanyua mashabiki wake dakika ya 41 akifunga bao safi kwa kichwa baada ya kupokea pasi kutoka kwa Shaban Djuma hilo ni bao lake la sita Msimu huo katika Ligi hiyo.
Baada ya Yanga kupata bao Coastal waliendelea kumiliki mpira hadi mwamuzi anamaliza kipindi cha kwanza Yanga walienda mapumziko wakiwa mbele ya bao moja kwa bila.
Kipindi cha pili kilianza kwa kila timu kufanya mabadiliko pamoja na kuendelea kushambuliana kwa zamu.
Mnamo dakika ya 90 Said Ntibazonkiza alipigilia msumari wa pili akimalizia pasi ya Farid Mussa na kuwanyamazisha mashabiki wa Coastal waliokuwa wamefurika uwanjani.
Kwa matokeo hayo Yanga wamefikisha Pointi 32 kwa michezo 12 na kuendelea kuongoza msimamo wa Ligi ya NBC nafasi ya pili Simba wakiwa Pointi 24 kwa mechi 10.
Matokeo mengine Timu ya KMC kutoka Kinondoni wameng’ara ugenini kwa kuichapa Tanzania Prisons mabao 2-0.
Ligi Kuu ya NBC itaendelea kesho kwa mchezo mmoja Mbeya City kuwakaribisha Simba katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.