………………………………………………………..
Nteghenjwa Hosseah, Dar es salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Innocent Bashungwa ametoa siku saba kwa tume iliyoundwa kuchunguza kuungua kwa soko la karume Jijini Dar es salaam kuhakikisha imekamilisha uchunguzi wake ili wafanyabiashara hao waweze kuendelea na shughuli zao za kujitaftia kipato.
Pia Waziri Bashungwa ameagiza Wakuu wa Mikoa kote nchini kufanya tathmini ya athari za moto kwenye wilaya zote na kuleta taarifa ndani ya siku 14 ili tuwe na mipango thabiti ya kuzuia ajali za moto katika maeneo yote.
Mhe. Bashungwa ametoa kauli hiyo alipofanya ziara kwenye Soko la Karume kuangalia athari ya moto huo na kutoa pole kwa wafanyabiashara walioathirika na janga hilo la moto.
Hapo awali Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makala alipofika kuzungumza na wafanyabiashara hao alitoa siku 14 kwa Tume kufanya uchunguzi wa kuungua kwa soko hilo.
Kutokana na malalamiko ya wafanyabiashara hao kuwa siku hizo ni nyingi kwa kuwa wanategemea eneo hilo ndipo Viongozi wakipokutana na Timu hiyo na kufanya mazungumzo na ndipo Waziri Bashungwa alipotoa maagizo ya kupunguza siku hizo kutoka 14 mpaka siku 7.
“Natambua hasara mliyopata kutokana na ajali hii na najua mnapategemea Soko hili kuendesha maisha yenu siku 14 ni nyingi hivyo nimeagiza Tume kutumia siku saba tu kukamilisha uchunguzi wao ili muweze kuendelea na biashara zenu’ amesema Mhe. Bashungwa.
Naye Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Ashatu Kijaji amesema Wizara yake itashirikiana na bega kwa bega na TAMISEMI kuhakikisha kuwa wafanyabiashara hao wanarudi kwenye hali zao za kawaida.
Pia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini ametoa pole kwa wafanyabiashara hao na kuahidi kuwa Wizara yake itashughulikia malalamiko yaliyowasilishwa.
Soko la Karumu lenye wafanyabiashara zaidi ya 500 lina historia ya kukabiliwa na majanga ya moto mara kadhaa na moto huu uliotokea kuanzia saa tisa usiku wa kuamkia leo ni tukio la tatu kutokea katika soko hilo.