…………………………………………………….
Adeladius Makwega,Moshi
Jumapili ya Januari 16, 2022 imenikuta katika Mji wa Moshi, kwa hakika nimekutana mazingira ya ukimya, utulivu na masafi. Ambayo sijawahi kukutana nayo kwa kipindi kirefu ambayo awali niliyaona katika Jiji ya Bonn-Ujerumani.
Mitaa ya Moshi hakukuwa na watu wengi zaidi ya vijana wa boda boda ambao wanatoa huduma hiyo. Huku kukiwa na milio ya bodaboda na magari hapa na pale. Nilitoka hapa nilipofikia na kumsimamisha kijana mmoja wa bodaboda ambaye nilimuomba anipeleke katika Kanisa Katoliki jirani. Kijana huyu hakufanya ajizi, aliwasha bodaboda yake na kuanza safari kanisani.
Tulifika katika Parokia ya Bikira Maria Malkia na Mama, Korongoni Jimbo Katoliki la Moshi. Nilimlipa bodaboda shilingi 1000 na kuingia kanisa. Nikiwa kanisani nilibaini kuwa ibada hii imejaa watoto wengi, wengine wakiwa wamevalia sare za shule. Huku watu wazima wakiwa wachache mno.
Ibada hii iliongozwa na Padri Deogratias Matihika. Kubwa kwa leo ni muujizi wa Yesu Kristu alipobadilisha mapipa ya maji na kuwa divai, ambapo Padri Matihika alisema kuwa maana yake hata sisi tukiomba kupitia kwa Mama Maria maombi yetu yatasikilizwa.
“Watoto mnasomeshwa na baba zetu ili mpate urithi wa elimu na siyo maduka au mashamba ya baba zenu. Unasema wewe hautaki kusoma kisa duka au shamba, hiyo haikubaliki kabisa, watoto someni, huo ndiyo urith wenu.” Alisisitiza Padi Matihika akihitimisha ibada hiyo.
Nikiwa katika ibada hiyo nilistajabishwa na watoto hao wadogo wakati wakiimba nyimbo zote wanajiongoza wao wenyewe, tangu kuimba sauti ya kwanza, ya pili, ya tatu, na ya nne na kupinga ala zote, kinanda, ngoma, kayamba na Isitoshe hata waongozaji wa nyimbo hizo walikuwa watoto.
Nikiwa kanisani hapo nilibaini pia namna waumini wanavyoshiriki kutoa sadaka ambapo kwa jumapili iliyotangulia walifikisha kiasi kinachozidi milioni 2.
Mara ibada ilipokwisha niliamua kurudi nilipofikia kwa kutembea kwa mguu, ili nijifunze namna Mji wa Moshi ulivyo lakini nilipotea njia kwa kutumia zaidi ya saa nzima, huku jasho likinitoka. Mwanakwetu! Kiranga cha kuufahamu Mji wa Moshi kilikwisha. Ndipo niliwatafuta bodaboda waliponiekeza vizuri na kurudi nilipofikia.
[email protected]
0717640257