……………………………………………………
Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dodoma
Watanzania tumeanza mwaka mpya wa 2022 kwa bashasha huku tukithamini na kuipenda nchi yetu adhimu ya Tanzania ambayo imebarikiwa kuwa na nyimbo nzuri ambazo ni Sala ama Dua ya kuliombea taifa na watu wake.
Wimbo wa Taifa pamoja na nyimbo za uzalendo zinakiri kuwa tuna nchi nzuri kama inavyosisitizwa na wimbo wa “Tanzama Ramani” ambao umeendelea kuwahimiza Watanzania kuwa wazalendo kwa nchi yao.
Wimbo wa taifa ama nyimbo za uzalendo lengo lake ni kuendeleza na kukuza uzalendo na utaifa ili kufanikisha maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa na kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya jemedari Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan za kujenga Taifa lenye utu, weledi na uadilifu.
Uzalendo ni hali ya mtu kuipenda, kuithamini na kujitoa kwa ajili ya nchi yake. Hali hiyo inamfanya mzalendo wa kweli daima kuipenda nchi yake na kuyapa kipaumbele maslahi ya nchi na kuyaweka maslahi yake binafsi nyuma.
Hali hiyo inadhihirishwa na Kiongozi Mkuu wa nchi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye kila mara amekuwa akiwahimiza Watanzania kuendeleza utamaduni wa taifa wa kushikamana, kupendana na kushirikiana ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa ya amani na utulivu.
Wimbo wa Taifa hili ni dua ya kuliweka taifa mikononi mwa Mungu kuanzia bara zima la Afrika, viongozi pamoja na watu wake wakiongozwa na tunu za hekima umoja na amani ambazo ni ngao zinazotumiwa na watoto wa Afrika kulifanya bara hili kuwa sehemu salama ya kuishi pamoja ambayo tangu awali imekuwa ndoto ya waasisi ya mataifa mengi ya Afrika akiwemo Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (13 Aprili 1922 – 14 Oktoba 1999), Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hiyo haikuwa ndoto ya Mwalimu Nyerere peke yake kuifanya Afrika kuwa moja, bali wapo viongozi lukuki wa bara hili ambao azma ya uzalendo kwao ilikuwa ni kujenga Umoja wa Muungano wa Afrika (OAU) uliokuwepo tangu mwaka 1963 na sasa Umoja wa Afrika (UA) unaohusisha nchi 55 ulioanzishwa Julai 2002.
Kwa uchache viongozi hao ni Kwame Nkrumah (21 Septemba 1909 – 27 Aprili 1972) Rais wa kwanza wa Ghana na mmoja wa viongozi waliokuwa na nia ya kujenga Muungano wa Afrika, Mfalme Haile Selassie wa Ethiopia (Julai 23, 1892 – August 27, 1975), Robert Gabriel Mugabe (21 Februari 1924 – 6 Septemba 2019) Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Zimbabwe, Nelson Rolihlahla Mandela (18 Julai 1918 – 5 Desemba 2013) Rais wa kwanza wa Afrika Kusini na Muammar al-Gaddafi (7 Juni 1942 – 20 Oktoba 2011) aliyekuwa kiongozi wa taifa la Libya.
Dhamira ya viongozi hawa mara zote imezingatia misingi ya utawala bora. Kwa Tanzania hali hiyo inadhihirishwa kupitia wimbo wa taifa katika ubeti wa pili ambao unaliweka taifa mikononi mwa Mungu na kuwahimiza Watanzania dumisha uhuru na umoja kwa watu wote, wake kwa waume na watoto ili kujenga nchi yenye mshikamano miongoni mwa watu wake.
Ni ukweli usiopingika dua ama sala hii inaendelea kuimarisha utamaduni wa taifa ambao umejengwa kwenye msingi imara kwa kuzingatia tunu za amani, umoja na mshikamano na uhuru wa nchi ambazo zinaendelea kulindwa na kudumishwa kwa manufaa ya Watanzania, Afrika na dunia nzima.
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema “Utamaduni ni kiini ama roho ya Taifa lolote. Taifa lisilo na utamaduni ni sawa na mkusanyiko wa watu wasio na roho.”
Haya ni maneno ya hekima ambayo yanajenga kuthamini vya kwetu ndiyo maana nyimbo maarufu za kujenga uzalendo miongoni mwa Watanzania zinaendelea kuwa lulu ya kujenga hamasa kwa watoto wadogo hadi watu wazima.
Wimbo wa Tazama ramani utaona nchi nzuri, umekuwa sehemu adhimu ya hamasa kwa watanzania kuipenda nchi yao kwa kuwaonesha uzuri wake na madhari nzuri yenye kuvutia yenye uoto wa asili ukipambwa na mito, bahari, milima, nyika, mbuga na mabonde ambavyo vyote vimekuwa na manufaa kwa nchi na watu wake ndiyo maana wimbo huo unasisitiza “Nasema kwa kinywa, kwa kufikiri, nchi hiyo mashuhuri huitwa Tanzania”.
Wimbo huo unaongeza kuwa Tanzania imekuwa Chemchem ya furaha na amani yenye kuleta tumaini, nchi yenye azimio lenye tumaini na mwanga wa Watanzania ambao wanauthamini hadharani na moyoni na hatimaye kuwa tayari kuilinda nchi yao wanayoipenda.
Ndiyo maana wimbo wa Tanzania Tanzania, nakupenda kwa moyo wote, unaendelea kuwahimiza Watanzania kuwa watu wema sana na nchi yao kwa kuwa ina jina tamu sana ambapo kila wakilala wanaiota, waamkapo ni heri na kuipenda kwa moyo wote na nchi nyingi zakuota, wageni wengi huja nchini kwa kutalii, kuwekeza pamoja na kufanya kazi mbalimbali.
Ujio wa wageni hawa wawe watalii wa kiutamaduni ama kwenye shughuli nyingine za kijamii, huchangia kuimarisha ushirikiano katika kujenga uchumi wa nchi na kuwa chanzo cha mapato kwa taifa na watu wanaotoa huduma kwa wageni hao ndiyo maana sehemu ya ubeti wa tatu inakiri kuwa “Na wageni wa kukimbilia ngome yako imara kweli wee, Tanzania Tanzania, Heri yako kwa mataifa”.
Hatua hiyo ya ukarimu wa taifa umeijengea Tanzania heshima miongoni mwa mataifa na mashirika ya kimataifa kuwa ni taifa linalojali watu na utu wao ambapo wimbo huo unazidi kuwa sehemu mujarabu ya kuliombea taifa ndiyo maana unahimza kuwa “Mola awe na we daima.”
Ndiyo maana Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa anawasisitiza Watanzania kuwa “Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan ana matumaini makubwa kwa Watanzania wote, tuendelee kuliombea Taifa letu na kila mmoja ashiriki katika shughuli za maendeleo, hatua tunayotarajia itafikishwa na sisi wenyewe tutafanikiwa sana kwa kuzingatia haya.”
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa mara baada ya kuapishwa kuiongoza wizara hiyo ameudhihirishia umma wa watanzania kuwa wizara hiyo ni nyeti kwa kuwa inasimamia maadili ya mtanzania na inadhamana ya kuwapa watanzania furaha, starehe, burudani, raha pamoja na kuutangaza utamaduni wa mtanzania kimataifa na Serikali inajua unyeti wa Wizara hiyo na kuithamini.
Kauli hiyo ya Waziri Mhe. Mchengerwa inaleta matumaini na imani kubwa ya kuendelea kuwahimiza Watanzania kuzingatia mila na desturi, maadili na utamaduni wa Mtanzania hususan kwa vijana, hatua inayosaidia kuhamasisha wananchi kuthamini na kuendeleza utamaduni wao na kuurithisha kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Ndiyo maana Watanzania pamoja na vikundi mbalimbali wamekuwa mstari wa mbele kudumisha Utamaduni na Sanaa ambazo ni sekta zinazoleta chachu na hamasa ya uzalendo kwa nchi ndiyo maana Band ya Atomic Jazz katika wimbo wao wanasema “Tanzania yetu ni nchi ya furaha”.
Huu ni mfano halisi wa kazi za Sanaa ambazo zinashuhudia Tanzania kuwa ni nchi ya kusifiwa pote ulimwenguni na watu wote wanatambua kuwa Tanzania ndiyo nchi yenye furaha na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia salamu ya “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, inasisitiza kuwa “Kazi Iendelee.”