Mwenyekiti wa Jukwaa la Wadau wa Maji Bodi ya Maji Bonde la Kati Msaru Msengi.akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Kaimu Mkurugenzi Rasilimali za Maji na Mwenyekiti wa Mabonde yote Tanzania na Afisa wa Maji Bonde la Pangani, Segule Segule akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Wadau wa maji wakiwa katika picha ya pamoja. Kutoka kushoto wakiokaa ni Kaimu Afisa Maji Bonde la Kati Danford Samson, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wadau wa Maji Bodi ya Maji Bonde la Kati Msaru Msengi na Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida katika uzinduzi huo, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Mang’alu Butondo.
Na Godwin Myovela,
Singida.
JUKWAA la pili la wadau wa maji Bonde la Kati limekutana
mkoani hapa kujadili mambo kadhaa ikiwemo namna bora ya kukabiliana na
changamoto za kupungua kwa vyanzo vya maji juu na chini ya ardhi na namna bora
ya kukabiliana na hali hiyo kwa ustawi na mustakabali wa watu na wanyama
waishio ndani ya bonde hilo ambalo ni la pili kwa ukubwa likitanguliwa na Bonde
la Rufiji.
Wadau hao kutoka kundi la watumia maji binafsi, Jumuiya za
watumia maji, Halmashauri za Wilaya, Mamlaka za Maji, Wakala wa Maji na Usafi
wa Mazingira Vijijini, Sekta zinazohusiana na maji, Wizara ya Maji na Bodi za
Maji za Mabonde, pamoja na mambo mengine, walipata fursa ya kupendekeza majina
ya Wajumbe wa Bodi ya Sita ya Maji ya Bonde la Kati baada ya iliyokuwa bodi ya
Tano kumaliza muda wake.
Pia kupitia kikao hicho wadau hao wa rasilimali za maji kwa
pamoja walipitia mpango mkakati waliojipangia kuutekeleza katika Jukwaa la kwanza
sambamba na kuandaa na mpango mkakati mwingine utakaotekelezwa katika kipindi
cha mwaka mmoja kuanzia sasa.
Akizungumza jana wakati akizindua Jukwaa la Pili la Wadau wa
Maji Bodi ya Maji Bonde la Kati, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Dk. George
Lugomela, kwa niaba ya Katibu Mkuu, alisema sheria, kanuni na miongozo
mbalimbali imeandaliwa na ipo kisheria huku mingine ikiwa mbioni kukamilika
lengo hasa ni kuendelea kuelekeza kwa kina jinsi ushiriki wa wadau wa sekta
mtambuka unavyotakiwa kuzingatiwa katika ulinzi, uhifadhi, utunzaji na
uendelezaji wa rasilimali za maji.
Lugomela katika mkutano huo uliobebwa na kauli mbiu ‘Vyanzo
vya Maji, Uhai Wetu, Tuvitunze’ alisisitiza kwa kuwasihi wadau wa majukwaa hayo
kushiriki kikamilifu katika kutekeleza shghuli zilizoainishwa kwenye mpango wa
usimamizi wa pamoja wa rasilimali za maji bonde kwa tija inayolenga kuleta
ustawi na uendelelevu wa rasilimali hiyo muhimu.
“Sasa tunapaswa kujikita zaidi kwenye kuyatambua mabonde
madogo (vidaka maji) kwa maana ya kuzindua majukwaa mengi zaidi kwenye ngazi
hii sambamba na kuyawekea utaratibu mzuri wa kisheria ili kuwezesha usimamizi
thabiti wa mpango jumuishi uliopo wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za
maji Bodi ya Maji Bonde la Kati,” alisema Lugomela
Hata hivyo Katibu Mkuu aliitaka ofisi ya bodi ya maji ya
bonde hilo na mabonde mengine nchini
kuanza kuangalia uwezekano wa kupanga na kuweka mikakati ya pamoja
kuhakikisha majukwaa yote kuanzia ngazi ya taifa mpaka chini yanaanza
kujiendesha chini ya uratibu wa kitaalamu wa wizara.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wadau wa bonde hilo
Msaru Msengi alisema kwa sasa bodi hiyo inakabiliwa na changamoto ya
uhaba wa vyanzo vya maji juu na chini ya ardhi hivyo kila mdau anawajibika
kushiriki ipasavyo katika uhifadhi wa vyanzo vilivyopo.
“Kulingana na athari za mabadiliko ya tabia nchi vina vingi
vya maji huenda vikaendelea kukauka au kupungua sasa ni jukumu la kila mmoja
wetu kujikita katika kukabiliana na changamoto hizo ambazo zinaweza kuathiri
watu wetu na wanyama tulionao ambao idadi yake ni kubwa ndani ya bonde hili,” alisema.
Awali, Kaimu Afisa wa Maji Bonde la Kati, Danford Samson
pamoja na mambo mengine, alisema bodi hiyo mpaka sasa kwa kushirikiana na wadau
imefanikiwa kuitisha jukwaa hilo kwa lengola kuweka mikakati na mpango kazi wa
kushughulikia matatizo na changamoto zilizopo, kuandaa na kutekeleza Mpango
Mkakati wa Bodi wa miaka 5, pamoja na kuandaa na kutekeleza mpango wa usimamizi
wa pamoja na uendelezaji wa rasilimali za maji wa miaka 20.
“Kwa sasa tunaendelea na mchakato wa kuandaa mpango wa
uhifadhi wa vyanzo vya maji (catchment conservation plan) na kutekeleza
majukumu mengine ya kisheria ya bodi ya maji unaofanywa kupitia Sera ya Maji ya
mwaka 2002 pamoja na Sheria ya usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya mwaka
2009,” alisema Kaimu huyo Afisa wa Maji Bonde la Kati.