*************************
Na Mwamvua Mwinyi, Kisarawe
WAKAZI wa vijiji 17 ikiwemo Chang’ombe, pamoja na kata ya Masaki Tarafa ya Sungwi ,wilayani Kisarawe Mkoani Pwani, wanatarajia kuondokana na kero ya kutembea masaa matatu kwenda kufuata maji visimani changamoto ambayo inawakabili toka Uhuru.
Wakazi hao wamekuwa wakitaabika kufuata maji umbali mrefu, na wengine kujiamulia kuchimba visima visivyo salama kwa afya zao kisha kuweka maji shabu ili waweze kutumia kwa matumizi ya nyumbani na kunywa.
Wakazi wa Sungwi Hadija ,mzee Suleiman,na Amina ,waliiomba Serikali iwasaidie waweze kupata maji .
Kufuatia kilio hicho, Waziri wa maji ,Jumaa Aweso alisema maeneo hayo yatapata maji kupitia mradi wa maji Kazimzumbwi-Changombe A utakaogharimu Bilioni 18.8 ambapo kwasasa Serikali inakabidhi mradi huo kwa Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA )baada ya hatua ya usanifu kutoka kwa RUWASA.
Alisema , Serikali inaendelea kutatua kero ya maji na itahakikisha inamtua ndoo mama kichwani.
Aweso alibainisha, DAWASA imefanya kazi nzuri , Mtendaji mkuu nakukabidhi mradi huu mkauendeleze ili kuondoa changamoto ya maji kwa wakazi wa maeneo hayo ya Sungwi,Masaki ,Chang’ombe A.
Nae Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Selemani Jafo alieleza, Serikali imeweka historia wilaya ya Kisarawe kwa miradi ya maji ,kwani wilaya ilikuwa na kero kubwa ya maji.
“Serikali imeleta mradi mkubwa wa maji kutoka Kibamba -Kisarawe kwa gharama za Bilioni 10.6 na kuzalisha Lita milioni sita za maji kwa siku”
“Waziri huyu nimemuomba ,aje la zaidi Ni kuja kuzungumza na wananchi wa Sungwi ili kuwaeleza namna Serikali itakavyotatua tatizo la maji, nimemuomba kuja hapa kwa Jambo moja ,Maji eneo hili halina maji ,Nimemwambia Kuna shida ya maji na mradi huu upo chini ya RUWASA “
Jafo alieleza kamuomba Waziri kazi hiyo ishughulikiwe na DAWASA kwakuwa RUWASA misuli ni midogo ,ili DAWASA imalize kero hiyo ya maji katika maeneo hayo hadi Kijiji Cha Kikwete kipate maji.
Mtendaji mkuu DAWASA , Mhandisi Cyprian Luhemeja amepokea maelekezo na kusema kazi Ni rahisi kuianza na atazungumza na RUWASA kujua kazi ilipofikia ili waendelee na utekelezaji .
Meneja wa RUWASA Kisarawe ,Majid alifafanua kutokana na kero hiyo Serikali kupitia RUWASA kwa kushirikiana na DAWASA inatekeleza mradi wa maji Kazimzumbwi-Masaki Chang’ombe, unaotarajiwa kuanza April mwaka huu na utatekelezwa kwa miezi 18 ,na utatumia Bilioni 18.8 .
Alisema, mradi huo Ni upanuzi wa mradi wa Mkubwa wa Kibamba -Kisarawe utachukua maji chanzo cha bomba kubwa la DAWASA, mradi wa Kibamba-Kisarawe.
Majid alieleza,kwasasa hatua inayochukuliwa ni wanatafuta mkandarasi na mradi utanufaisha wakazi 38,000 katika vijiji 17.
“Eneo hili linakabiliwa na kero ya maji kwa miaka mingi,maji safi na salama wanayasikia kwa wenzao ,kwa hatua hii , upatikanaji wa maji utakuwa kwa asilimia 21 “