Ofisa madini mkazi wa Mirerani (RMO) Fabian Mshai akizungumza na wamiliki wa migodi na mameneja wa migodi ya Tanzanite, kushoto ni Katibu wa MAREMA Tariq Kibwe na Ofisa mkaguzi wa migodi Castro Maduwa.
****************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAMILIKI wanaochimba migodi ya madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kulipia leseni wanazozimiliki ili waendelee kufanya kazi.
Zaidi ya migodi 2,000 ya madini ya Tanzanite imekatiwa leseni ya uchimbaji ila iliyopo hai na inayofanyiwa kazi ni migodi 300 pekee.
Ofisa madini mkazi wa Mirerani Fabian Mshai ameyasema hayo juzi wakati akizungumza na wamiliki na mameneja wachimbaji wa madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani.
Mshai amesema wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite, wanaodaiwa fedha za leseni zao wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa kulipa ili kuondokana na kufuatanafuata.
Amesema leseni zisipofanyiwa kazi zinasababisha madeni kwani wanapoomba wanapaswa kuziendeleza kwa kuhakikisha zinafanya kazi.
“Hivi sasa kuna madeni mengi ya fedha za leseni takribani sh300 milioni hivyo wale wote wanaodaiwa wafike ofisini ili walipe na kuendeleza sekta,” amesema Mshai.
Katibu wa chama cha wachimbaji wa madini mkoa wa Manyara (Marema) Tariq Kibwe amesema suala la wachimbaji kulipia leseni zao halikwepeki hivyo watekeleze suala hilo.
Kibwe pia amesema wachimbaji madini wanapaswa kuwajali wafanyakazi wao pindi wanapougua na siyo kuwatelekeza.
Ofisa mkaguzi wa migodi mhandisi Castro Maduwa amesema wachimbaji wanaponunua zana za milipuko wanapaswa kuwa na vibali ili watambulike na pia waepushe ajali zisizokuwa za lazima.
Amesema wanaponunua zana za milipuko wanatakiwa kuorodhesha vifaa wanavyohitaji ili waweze kuvinunua.
Mwenyekiti wa Tanzanite, Money Yusuf amesema mchimbaji anapaswa kuzingatia agizo la kuwa na kibali cha milipuko kwani wanaweza kukamatwa na serikali.