…………………………………………………
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Shinyanga wameeleza sababu zinazochangia kutengana kwa wanandoa kuwa ni pamoja na utandawazi na ukosefu wa maadili mema hasa kwa vijana.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema kumekuwa na wimbi la wanandoa kutokudumu kwa muda mrefu na kwamba kanuni na taratibu zilizowekwa kwa baadhi ya wanandoa hazizingatiwi.
Wananchi hao wameeleza kuwa kumekuwa na utofauti kati ya ndoa za zamani na za sasa ambapo wamesema changamoto kubwa kwa wanandoa ni tamaa, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na kutoaminiana hasa kwa vijana.
Wameongeza kuwa kutokuwa na hofu ya Mungu, kukosa maadili mema inachangia kutokuwa na uvumilivu katika ndoa hivyo wameshauri kila mtu kusimama imara katika kujenga ndoa yake ili kudumu kwa muda mrefu.
Kwa upande wake mchungaji wa kanisa la Waadventista wa Sabato lililopo kata ya mjini katika Manispaa ya Shinyanga Mchungaji Lazaro Mbogo na ni mjumbe wa kamati ya amani mkoa wa Shinyanga amesema ndoa nyingi zinazofungwa zina changamoto mbalimbali ambazo zimekiuka maadili ambapo amesema ndoa za zamani za kimili wazazi walihusishwa kwa karibu sana.
Amesema baadhi ya wanandoa hawaoani kwa upendo wa dhati hivyo amesema wanaoana kwa tamaa za kimwili zisizo kuwa na tija kwenye ndoa.
Mchungaji Mbogo ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya amani mkoa wa Shinyanga amewashauri wananchi kumshirikisha Mungu pamoja na viongozi wa dini katika masuala ya ndoa ili kujenga ndoa Imara.
“Nini ambacho kinaweza kufanyika katika kipindi hiki kabla ya wanandoa kufunga ndoa na kuamua kuishi pamoja wamshirikishe Mungu jambo la pili watushirikishe sisi ambao ni walezi wa kiroho wachungaji kwa kuwauliza maswali na kuwashauri juu ya safari yao ya ndoa na yale yatakayowapata kule mbele waone kama wanashindwa ni bora wasionane badae wakaleta aibu ya kutengana maana wanaoana anazani atamuacha huyu ataoa mwanamke mwingine sasa haya mambo yasipochukuliwa hatua mapema yatapokelewa kwamba kuolewa na kuachana ni jambo la kawaida na madhara yake nchi yetu inaweza kuingia kwenye ndoa za mkataba miezi miwili mitatu jambo ambalo ni hatari”.
Aidha mchungaji huyo ameomba ushirikiano kwa viongozi mbalimbali wanaofungisha ndoa hawa viongozi wa serikali mawakili pamoja na maafisa ustawi wa jamii pale wanapopata kesi za kutengana kwa wanandoa wawashirikishe wachungaji ili kuepusha wimbi hilo la kutengana kwa wanandoa.