Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo akihutubia wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha Walimu Wakuu na Wahasibu wa Shule za Sekondari zinazomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania katika Ukumbi wa NEC, Makao Makuu ya CCM Dodoma. (Picha na Adam Mzee)
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi (Zanzibar) Ndugu Othman A. Maulid akitoa salaam za shukrani mara baada ya ufunguzi wa Kikao Kazi cha Walimu Wakuu na Wahasibu wa Shule za Sekondari zinazomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania katika Ukumbi wa NEC, Makao Makuu ya CCM Dodoma. (Picha na Adam Mzee)
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Ndugu Gilbert Kalima akizungumza wakati wa Kikao Kazi cha Walimu Wakuu na Wahasibu wa Shule za Sekondari zinazomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania katika Ukumbi wa NEC, Makao Makuu ya CCM Dodoma. (Picha na Adam Mzee)
…………………………………………..
Na.Elisa Shunda, Dodoma
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Daniel Chongolo, amepiga marufuku tabia ya shule za jumuiya kutumika kama viwanja vya kampeni wakati wa vipindi vya uchaguzi sababu suala hilo linaathiri shule.
Chongolo ameitoa kauli hiyo leo Januari 14,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye mkutano wa wakuu na wahasibu wa shule za Jumuiya hizo wenye lengo la kujadili kuhusu usimamizii wa shule za jumuiya, uendeshaji wake, na usimamizi wa rasilimali za shule na fedha.
“Tuache kutumia shule zetu Kama majukwaa ya kufanyia siasa za uchaguzi, maana inaathiri shule zetu fanyeni mapitio jiangalieni mnavyoenda halafu mjipime, acheni shule ijitangaze yenyewe kiutendaji, tengenezeni mifumo pambaneni ili mtoke sehemu moja kwenda nyingine tutakuwa wakali tukishindwa tutabadilisha matumizi ya shule zetu au tuone namna nyingine ya kuendesha shule zetu,” Alisema Chongolo.
Aidha, ametishia kuzifuta shule za Jumuiya ya chama ambazo zinaonekana mzigo kwa kufanya vibaya kwenye matokeo ya mitihani huku akitoa mwaka kwa wakuu wa shule hizo kubadilika.
Pia, ametahadharisha kuhusu ugonjwa wa shule hizo kutofikisha taarifa za fedha makao makuuu ya Chama na kuonya mali za jumuiya kutoliwa na watu binafsi kwa kuwa atakua mkali katika kusimamia mali hizo akishirikiana na katibu mkuu wa jumuiya ya wazazi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi, Ndugu, Dkt.Edmund Mndolwa, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi, Ndugu, Gilbert Kalima, Manaibu wa Jumuiya Hiyo, Ndugu, Daniel George Sayi (Bara), Ndugu, Othman Alli Maulid (Zanzibar), Wakuu wa Shule za Sekondari za Jumuiya ya Wazazi na Wahasibu.