Mkuu wa wilaya ya Arusha, Said Mtanda akizungumza katika kikao hicho jijini Arusha leo.
Afisa uhusiano wa AUWSA , Masood Katiba akiwasilisha mada katika kikao huo.
Wadau mbalimbali wakiwa katika kikao cha ushirikishwaji wa kukusanya maoni juu ya maandalizi ya mkataba wa huduma kwa mteja kilichoandaliwa na AUWSA Leo jijini Arusha.
*************************
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Mkuu wa wilaya ya Arusha,Said Mtanda ameitaka mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira jiji la Arusha kuendelea kuelimisha wananchi juu ya matumizi sahihi ya huduma za maji na majitaka ili kuepuka malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa kutokana na ukosefu wa elimu hiyo.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza katika.kikao cha wadau katika ushirikishwaji wa kukusanya maoni juu ya maandalizi ya mkataba wa huduma kwa mteja kilichofanyika mjini hapa.
Amesema kuwa,ni lazima mamlaka hiyo iende kwa wananchi wenyewe na kutoa elimu badala ya kukaa na kusubiri malalamiko yawafikie ofisini ,Jambo linalosababishwa na kutokuwepo kwa elimu ya kutosha kwa wananchi hao ambao ndio watumiaji wakuu wa maji.
“Naombeni sana msikae kusubiri malalamiko yawafuate badala yake hakikikisheni mnatenga muda na kuwafuata wananchi katika maeneo yao ili muweze kubaini changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi wa haraka”alisema Mtanda.
Aidha ameitaka mamlaka hiyo kutoa taarifa kwa wananchi juu ya gharama sahihi zinazostahili kutumika kwa kutumia lugha inayoeleweka kwani imekuwa ni changamoto kubwa kwa wananchi kutokuelewa kiwango sahihi cha matumizi ya maji wanachotumia.
Hata hivyo alitaka kuwepo kwa lugha nzuri na mapokezi mazuri kwa wateja pindi wanapofika kwenye mamlaka hizo huku akiwataka kuhudumia wateja kwa umakini na kupewa kipaumbele huku akitaka kuwasilishwa kwa taarifa zote kuhusiana na maendeleo ya maji na majitaka kwa wananchi na kwa wakati.
Naye Afisa uhusiano wa AUWSA,Masood Katiba akiwasilisha mada ya mkataba wa huduma kwa mteja Masood Katiba amesema kuwa,AUWSA imeandaa mkataba huo wa huduma kwa mteja ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yaliyoko chini ya sheria ya majisafi na usafi wa mazingira no 5 ya mwaka 2019 na maagizo kutoka kwa serikali kupitia wizara ya maji pamoja na mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji EWURA.
Amesema kuwa, mkataba huo wa huduma kwa mteja unatoa na kubainisha wajibu wa AUWSA kwa wateja ili kufikia lengo kuu la kutoa huduma endelevu za majisafi na usafi wa mazingira pamoja na kutoa mwongozo wa wajibu wa mteja katika kupokea huduma zitolewazo na AUWSA.
Katiba amesema kuwa,mamlaka inawasilisha mkataba huo ikitarajia kuwa utakuwa mwongozo sahihi na kuiwezesha mamlaka kushiriki kikamilifu katika kuboresha huduma zake,ili kuweza kufanya kazi vizuri mkataba huo inabidi uwe hati hai itakayowezesha kuleta mabadiliko katika utoaji wa huduma kwa kuwashirikisha wateja na wadau kwa kupata maoni na mapendekezo ili kujenga uhusiano mzuri na mteja.
“Madhumuni ya mkataba huu ni kumwezesha mteja kujua huduma zinazotolewa na viwango vya huduma hizo,mkataba huu pia unaelezea muda ambao mamlaka itatumia kutoa huduma na majukumu au wajibu wa mteja katika kupata huduma husika “amesema Katiba.
Nao baadhi ya wananchi wakichangia mada katika kikao hicho ,Mwenyekiti wa mtaa wa Long dong kata ya Sokon 1,Ibrahimu Mkuruzi amesema kuwa,wanaomba mkataba huo wa huduma kwa mteja uweze kuboresha mazingira kwa wananchi wanaotoka Kaya maskini ambao hawana maji kabisa kutokana na uwezo wao mdogo na kushindwa kupata maji,hivyo waliomba wananchi hao kupewa kipaumbele na kupewa maji bure kutokana na mazingira wanayotoka.