**********************
Adeladius Makwega
Dodoma.
Niliamka mapema siku ya Januari 10, 2022, kuelekea barabarani. Nilipofika kituo cha basi nilibaini kuwa barabara ya Buigiri Chamwino Ikulu ilikuwa na magari mengi yanayotoka mjini kuelekea Chamwino Ikulu, wakati kwa desturi magari mengi huwa yanatoka Chamwino Ikulu kuekea mjini wakati wa asubuhi na mchana hadi jioni huwa mengi kurudi Chamwino.
Leo kulikoni?
Nilishuhudia gari za kila aina za kiserikali, mabasi yaliyobeba watu kadhaa yalikuwa yakiingia ndani ya Ikulu yetu ya Chamwino. Nilikaa kituoni kwa dakika kama sita, mara ilikuja dalalada na mie kupanda hadi Mtumba njia panda ya Mji wa Kiserikali.
Nilishuka na kupanda bodaboda hadi Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, huku nikiona watumishi wakiwa na kazi zao za hapa na pale. Lakini taswira ilikuwa kama kuna jambo.
“Jamani hivi mnakumbuka kuwa leo Mheshimiwa Waziri Mchengerwa anakuja, mmeshajiandaa kumpokea?”
Priscal Shewali (Msambaa wa Gare Lushoto Tanga) ambaye ni Afisa Utumishi Mkuu alituuliza tuliowakuwapo.“ Ndiyo tunakumbuka na tupo tayari.” Alijibiwa.
“Jamani naombeni msiniangushe, Shamimu Nyaki(Msambaa-Mbugu) utampokea mgeni na kumkabidhi kadi na maua, naomba usitetemeke, maana yale mambo hayahitaji watu waoga, siyo unatetemeka alafu unaangusha kadi na ua letu chini.” Alisema kwa utani lakini akimaanisha hilo linalotamkwa Afisa Utumishi Mkuu Bi Shewali.
Alipoodoka, huyu mwenzetu Bi Nyaki, mara alipigiwa simu kwake na kujulishwa kuwahi nyumbani kwenda kumnyonyesha mtoto wake. Kwa hiyo hakujaliwa kumkabidhi mheshimiwa kadi na ua hilo na zoezi hilo alipewa mtumishi mwingine.
Karibu karibu karibuuuu uuuu karibuuu,
Viongozi wetu, karibuuu uuuu karibu
Karibu Mchegerwa
Karibuuu uuuu karibu,
Karibuu Yakubu
Karibuuu uuuuu karibu.
Nilisikia wimbo huo ukiimbwa kwa nguvu nje ya wizara hii. Mwanakwetu nilitoka nje kutazama kulikoni? Niliona watumishi wa wizara hii wanaojihusisha na hamasa wakiwa wamevalia khanga, vibwebwe wakiimba kwa bashasha. Mie nikaingia ulingoni kuimba japokuwa nilikuwa nakosea maneno maana nilikuwa sifahamu kwa kupachika Mchegerwa wala pa kupachika Yakubu.
Karibuuuuu uuuuuu, Karibu.
Wageni wetu
Karibuuu uuuu, Karibu.
Nilikuwa naimba hivyo tu na ilipotimu majira ya saa 8.27 mchana huku jua kali likiwaka Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa, Mohammed Omary Mchengerwa ambaye ni Mbunge wa Rufiji alishuka katika gari, akiwa mwenye furaha sana, alivalia suti ya rangi ya kijivu na miwani miyeusi.
Watumishi wa wizara hii wakiongozwa na Naibu Waziri Bi Pauline Gekul ambaye alivalia Suti Gauni jeusi yenye vibwebwe mkononi na barakoa mdomoni walimlaka kwa heshima na taadhima waziri wao.
Mheshimiwa Mchengerwa alipokabidhiwa ua na kadi, aliusalimu umati wa watumishi hao kwa kuwapungia mkono na kuingia katika wizara yake hii kwa hatua kubwa kubwa, kiukakamavu kana kwamba watu wanapima ekali ya shamba lenye hatua sabini kwa sabini. Kaa kaa kaa kaaa… hatua hizo zilisikika na kutoa taswira kuwa kweli mheshimiwa huyu ametoka kula kiapo kwa mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan Chamwino Ikulu, asubuhi ya siku hii.
“Kumbe mazingira ya wizara zetu zote yanafanana ehee! Kumbe ramani ni ile ile ehee.” Alisema Mheshimiwa Mchengerwa. Dkt. Hassan Abbas ambaye ni Katibu Mkuu wa wizara hiii alijibu.“Ni kweli na hapo pembeni tuna jengo linajengwa la ofisi zetu la ghorofa sita na ujenzi unaendelea.”
Aliingia ofisini kwake na kuketi katika sehemu ya makochi, kwanza aliweka saini katika kitabu cha wageni kwa kutumia mkono wake wa kulia, hiyo ikiwa ni ishara kuwa sasa amefika rasmi ofisini kwake.
Alipomaliza kusaini kitabu hicho alikabidhiwa Naibu Katibu Mkuu Ndugu Said Othumani Yakubu ambaye nayeye alitoka kula kiapo cha kuwa Naibu Katibu mpya wa wizara hii, Ndugu Yakubu aliyevalia suti ya rangi ya samawati, aliweka saini akitumia mkono wake wa kushoto.
Kwa hiyo kulia ya Waziri Mchegerwa na kushoto ya Naibu Katibu Mkuu Yakubu mambo yalikamilika na filimbi ya kuanza kwao kazi rasmi wizarani hapa ilikuwa imeshapigwa.
“Mheshimiwa karibu kwenye kiti chako.” Ilitamkwa na Naibu Wazuri Gekul.
Mheshimiwa Waziri Mchengerwa aliamka katika makochi na kuketi katika kiti chenye meza yake. Mara nikasikia milio ya kamera za wanahabari chawaa, chawaa, chawaa …angalau kupata picha ya mheshimiwa huyo.
Kweli zoezi hilo la mapokezi lilipokamilka na mie nilirudi zangu Chamwino, nako njiani nikikutana na ving’ora vingi barabarani kutambulisha kuwa leo Dodoma wakubwa wapo, leo Dodoma wakubwa wapo.