******************************
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limepokea kwa matumaini uteuzi wa Mhe. Nape Nnauye kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
TEF pia linamshukuru na kumpongeza kwa kuteuliwa katika Wizara nyingine, aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Ashatu Kijaji tuliyefanya naye kazi kwa karibu sana. Dk. Kijaji sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara.
Tunampongeza aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Dk. Jim Yonaz kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Tumefanya naye kazi vizuri na kwa ukaribu katika mchakato wa kurekebisha Sheria za habari, ambaye sasa tunaamini mchakato huu unaendelea kuwa katika mikono salama.
Tunampongeza Mohamed Hamis kwa kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Tunasema karibu sana.
Tunampongeza Dk. Zainab Chaula, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ambaye sasa ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Mahitaji Maalum.
Hakika Dk. Chaula alifanya kazi kubwa ya kupigiwa mfano hasa katika mchakato wa marekebisho ya sheria za habari na kuyarejeshea leseni magazeti yaliyofungiwa.
Hadi sasa utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya Juni 28, 2021 kuwa vyombo vya habari vilivyofungiwa vifunguliwe unaendelea kwa magazeti ya Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima.
TEF linampongeza Mhe. Rais Samia kwa kuunda upya Baraza la Mawaziri, na Jukwaa linaamini mawaziri walioteuliwa katika kila wizara watakuza Uhuru wa Kupata Habari, Uhuru wa Vyombo vya Habari na Uhuru wa Kutoa Mawazo, ambazo ni haki za msingi zinazowezesha haki nyingine kupatikana kwa mwanadamu, suala ambalo ni nguzo ya maendeleo ya kweli kwa kila nchi.
Tunamkaribisha Mhe. Nape katika wizara hii na tunaamini atatusaidia kusukuma kwa kasi mchakato wa kuyafungulia magazeti tuliyoyataja, huku akiupa msukumo mpya mchakato wa kubadili sheria zinazosimamia taaluma ya habari kwa nia ya kukuza Uhuru wa Vyombo vya Habari nchini.