……………………………………………………………………..
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Manyara, Kiria Kurian Laizer, ametimiza ahadi yake aliyoitoa hivi karibuni ya kuipatia shule shikizi ya Kandasikira ya Kata ya Shambarai, Wilayani Simanjiro mifuko 100 ya saruji.
Mwenyekiti wa UVCCM wa Wilaya ya Simanjiro, Thomas Mollel akikabidhi mifugo hiyo 100 ya saruji jana kwa niaba ya Kiria amempongeza kwa kutimiza ahadi yake aliyoitoa hivi karibuni.
Mollel amesema Kiria aliahidi kutoa mifuko hiyo ya saruji 100 kwa ajili ya kumalizia madaraja mawili ya shule hiyo shikizi ya Kandasikira, baada ya ziara ya siku moja ya kamati ya siasa ya CCM ya wilaya hiyo.
Amesema wadau wengine wanapaswa kumuunga mkono Kiria ili kufanikisha maendeleo kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo ya Simanjiro yenye changamoto tofauti.
“Ili wanafunzi waweze kusoma vizuri na kufaulu mitihani yao wanapaswa kusoma katika mazingira bora na yenye kutulia, kupitia mifuko hiyo 100 yatasaidia kuboresha shule hiyo,” amesema Mollel.
Ofisa mtendaji wa Kijiji cha Kandasikira, Habiba Njau akizungumza wakati akipokea mifuko hiyo 100 amemshukuru Kiria kwa kujitolea mifuko hiyo ya saruji.
Njau amesema shule hiyo shikizi inawatoto 400 ina madarasa sita na wanafunzi wapo kuanzia darasa la kwanza hadi la sita na mwaka huu wanatarajia kufanya mtihani wa darasa la saba.
“Tunaomba wadau wengine wa maendeleo waige mfano wa Kiria kwa kuchangia penye mapungufu ili kuiunga mkono serikali katika kuboresha miundombinu ya shule,” amesema Njau.
Mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Innocent Vitalis amesema ameungana na Mwenyekiti wa UVCCM wa wilaya hiyo kufikisha mifuko hiyo 100 iliyotolewa na Kiria.
Innocent amesema Kiria alitimiza wajibu wake kwa kukabidhi mifuko hiyo 100 ya saruji aliyoahidi kutoa baada ya kutembelea eneo hilo hivi karibuni akiwa na kamati ya siasa ya CCM Wilaya.