Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda akikagua maghala ya kuhifadhia mbolea ya Minjingu wakati alipofanya ziara ya kikazi katika kiwanda cha mbolea cha Minjingu Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Tarehe 7 Januari 2022.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Manyara
WAZIRI wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kutengeneza vipeperushi ambavyo vitasambazwa kwenye halmashauri za wilaya nchini ili kuitangaza mbolea ya hapa nchini.
Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 7 Januari 2022 wakati alipofanya ziara katika kiwanda cha Minjingu kilichopo Wilaya ya Babati mkoa wa Manyara akiongozana na Mkurugenzi wa Mazao Wizara ya Kilimo Ndg Nyasebwa Chimagu, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt Stephan Ngailo, Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI-Mlingano) Dkt Catherine Senkoro.
Profesa Mkenda amesema kwa sasa wanataka kufanya tathimini kama mbolea iuzwe nje kwa kiasi gani hususani ambayo haitumiki hapa nchini bila hivyo mantiki ya kiuchumi haina maana yoyote.
“Vipeperushi vitengenezwe na TARI mshirikiane na wenzenu muandike maneno tupeleke Mkoani haraka watu wajue ipi ya kuoteshea mazao gani na ndani ya wiki mbili tuwe tumehamasisha halafu tuangalie mbolea inakwenda kiasi gani tukiona kwamba bado ipo ya kutosha tutafanya tathimini haraka kwamba bado tuendelee kuzuia na tunazuia ili nini” Amekariwa Prof Mkenda
Aidha, amemtaka Mkurugenzi wa Maendeleo ya mazao kushirikiana na maafisa ugani kuwekeza maeneo yanayozalisha chakula kwa wingi ili kuondokana na hali ya utegemezi pindi kunapotokea changamoto ya chakula.
“Tutafute maeneo ya kufanya mbolea hii kama shamba darasa, tutangazie maafisa ugani Kwa kushirikiana na TARI na TFRA tutumie vipeperushi vya wizara kuitangaza mbolea ya ndani ya nchi ili kiwanda cha mbolea kifanye kazi vizuri” Amesisitiza Waziri Mkenda
Kiwanda kama hiki kisiposimama mkakati wetu hautaenda vizuri, kiwanda Cha mbolea kilichopo Dodoma tayari niliagiza Mkurugenzi wa Maendeleo ya mazao tumempeleka nchini Burundi kwenda kujifunza ndio amerudi nasubiri taarifa,” Amesema
Aliongeza: Nenda huko kaangalie mbolea kama tunaweza kununua kidogo lakini tuchukue uzoefu ambao tunaweza kutumia ili kama kile kiwanda kikifunguliwa tuwe na kauli ya kusema na sisi tumejaribu mahali flani tumeona efficiency yake, sasa hatuwezi kufanya hivyo Kwa kiwanda ambacho hakifanyi kazi.
Aliwahakikishia kuwa atazungumza na Katibu Mkuu ili kutafuta bajeti za kutengeneza vipeperushi ili kusambaza kwenye kila wilaya ili kuhamasisha vinawafikia watu wengi zaidi.
Awali, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Minjingu kilichopo Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Tosk Hans alisema wametii agizo la kupeleka mbolea ya kutosha mikoa ya Kanda ya kusini huku mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Songea, Rukwa, Sumbawanga yote ina mbolea ya kutosha ya kupandia na kulimia licha ya kuwa na changamoto ya mvua.
“Bei yetu ni rafiki hatutakuangusha kwani mkoa wa mbeya tumepeleka Tani 6200, mpaka mwisho wa msimu, tuna tani 1600 ambazo zipo mikoa ya kusini, huku tu angoja hadi msimu utakapoanza, ipo ya kutosha na bado ikihitajika tutapeleka na tuna tani 9000 zipo kwenye maghala hapa kiwandani ikingoja kwenda mahali popote itakapotokea changamoto ya mbolea,” Amesema Hans
Ameongeza kuwa hawakusafirisha mbolea nje ya nchi mpaka changamoto ya ndani iishe, hivyo kuomba mchakato huo uanze Kama wataruhusiwa.