***************************
Na. Damian Kunambi Njombe
Kutokana na baadhi ya taasisi za utoaji mikopo hapa nchini kuwahusisha askari polisi katika kufuatilia wadaiwa wao mkuu wa jeshi la polisi wilayani Ludewa Deogratius Masawe amewataka askari wake kutojihusisha na masuala hayo kwakuwa ni kinyume cha sheria.
Akizungumza na baadhi ya watoa mikopo wa taasisi mbalimbali wilayani humo afande Deogratias amesema taasisi hizo zinapaswa kutumia madalali wa mahakama katika kufuatilia madeni hayo badala ya kutumia polisi kitu ambacho ni kosa kisheria.
“Unakuta mtoa mikopo ana urafiki na askari mmojawapo hivyo anatumia njia hiyo kumtumia askari kwenda naye kudai madeni au kumkamata mdaiwa ili aweze kulipa mkopo wake, sasa napenda kuwajulisha kuwa huo ni ukiukwaji wa sheria na atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali kisheria”, amesena Masawe.
Ameongeza kuwa kila taasisi inapaswa kuwa na mkataba wa ukopeshaji na wakopaji wapewe kopi za mikataba hiyo ili watakapokiuka taratibu za mkataba huo waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria walizokubaliana badala ya kutumia askari kwenda kuwatishia na kuwanyanyasa wateja wao.
Sanjari na hili pia amezitaka taasisi hizo kutowakopesha askari yeyote atakayeenda kukopa bila kuwa na kibali kutoka katika uongozi wa jeshi hilo.
Amesema kumekuwa na kesi nyingi zinazohusisha mikopo kwa polisi lakini ukifuatilia mikopo waliyopewa inakuwa haijafuata taratibu sahihi na kuwaambia kuwa yeyote atakayetoa mkopo kwa askari hao bila kibali maalum endapo itatokea tofauti uongozi hauta usika kwa lolote.
Aidha kwa upande wa baadhi ya wakopeshaji hao wamedai kuwa wanatumia nguvu katika kudai madeni kutokana na wadaiwa wao kukaidi kulipa madeni yao kwa wakati na kuanza kuwasumbua.
Wamesema kwa elimu waliyoipata kutoka kwa mkuu huyo wa jeshi la polisi wameielewa na watajitahidi kufuata utaratibu sahihi katika utoaji huo wa mikopo.