***********************
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga inaendelea na mchakato wa kutoa mkopo kwa vikundi vilivyosajiliwa kwa ajili ya ununuzi wa magari yatakayotumika kusafirisha wanafunzi ili kupunguza au kuondoa kabisa changamoto ya kutembea umbali mrefu.
Mpango huo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwenye mahafali ya chuo cha ufundi stadi VETA baada ya wanafunzi kuwasilisha changamoto ya usafiri kupitia lisara yao kwa mgeni rasmi.
Akizungumza leo Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura amesema utekelezaji huo umeanza na kwamba tayari Halmashauri hiyo imetoa mkopo kwa vikundi viwili kwa vijana waliowasilisha maombi yao huku wakijadili maombi ya vikundi vingine viwili .
“Tunafahamu changamoto yao na siyo kwa VETA peke yao tu ni kwa wanafunzi wote ndani ya Manispaa ya Shinyanga ambao wanasafiri umbali mrefu kutoka majumbani kwao maeneo wanayoishi kuelekea shuleni na sisi kama Halmashauri tumeiona changamoto hiyo na tunasehemu ya mikopo tunatoa asilimia kumi tunataka vikundi vya vijana vinne waje wakope ili tuwapatie fedha wanunue gari kwa kuanzia tunaanza na gari nne na tayari vikundi viwili vimeshaleta maombi na tayari tumeshavipa fedha vikundi viwili vingine vimeleta maombi jana tutavijadilio leo ili tuvipatie fedha”.
Amesema malengo yao ilikuwa kufikia mwezi wa kumi na mbili mwaka jana 2021 gari hizo ziwe zimeanza kufanya kazi ambapo amesema vikundi hivyo vimechelewa kuwasilisha maombi hayo huku akisema mwisho wa mwezi huu au mwazo wa mwezi ujao 2022 gari ziwe tayari zimefika katika Manispaa ya Shinyanga”.
Bwana Satura amesema mpango huo ni endelevu na kwamba hatua hiyo itasaidia kupunguza au kuondoa changamoto hiyo ambapo ameomba ushirikiano zaidi ili mpango huo uweze kufanikiwa na kuondoa changamoto ya usafiri kwa wanafunzi katika Manispaa ya Shinyanga.
“Tutaendelea kutoa fedha kwa ajili ya vikundi viweze kununua gari na kubwa ambalo tunategemea kutoka kwao ni ushirikiano ili tuweze kusafiri safari yetu kwa pamoja”.
Mkurugenzi huyo bwana Satura amezitaka baadhi ya kata ambazo vitapewa kipaumbele katika usafiri huo ikiwemo kata ya Old Shinyanga, Kizumbi, Kolandoto na Mwawaza.