Na Godwin Myovela, Singida
WAKALA wa Maji na
Usafi wa Mazingira Vijijini Wilaya ya Singida mkoani hapa (RUWASA) imeanza kwa
kasi kutekeleza miradi mbalimbali ya usambazaji wa huduma za maji kwenye maeneo
kadhaa yanayozunguka wilaya hiyo ikiwemo vijiji vya Mitula, Mwiganji, Migugu na
Ughandi B ambavyo kwa muda mrefu vilikosa huduma hiyo muhimu.
Imeelezwa, kwa mujibu wa RUWASA Wilaya ya Singida zaidi ya
wananchi elfu kumi wanaozunguka vijiji hivyo wanatarajia kuanza kupata maji
safi na salama katika kipindi cha miezi mitatu mpaka mitano kuanzia sasa ikiwa
ni utekelezaji wa miradi minne ya kibajeti 2021/2022 chini ya serikali
inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo ya Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM)
Akizungumza jana muda mfupi baada ya kushusha mabomba na
vifaa vya mbalimbali vitakavyotumika kutekeleza mradi wa maji kwenye kijiji cha
Mitula na maeneo mengine, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Singida, Mhandisi Athuman
Mkalimoto, alipongeza kasi ya serikali na ushirikiano uliopo kwa namna
ilivyojikita kwenye umakini kuhakikisha huduma za usambazaji maji vijijini
zinaendelea kuimarika.
Meneja Mkalimoto alisema katika kutekeleza bajeti kwa mwaka
wa fedha 2021/22 RUWASA Wilaya ya Singida tayari imeanza kutekeleza mradi wa
maji kijiji cha Mwighanji ambao mpaka kukamilika kwake unatarajia kutekelezwa
kwa thamani ya shilingi milioni 500, huku mradi mwingine ambao tayari umeanza
kutekelzwa kwa hatua za mwanzo ni wa kijiji cha Migugu kupitia fedha za ‘Uviko’
unaokwenda kunufaisha zaidi ya wananchi elfu 6 ambao una thamani ya shilingi
milioni 565.
Alisema mradi mwingine wa kijiji cha Ughandi B mpaka sasa
tayari umeshatekelezwa kwa zaidi ya asilimia 75 ya ujenzi wake, na alisisitiza
kwamba kilichobakia ni ukamilishaji wa tenki la maji ili huduma zianze
kupatikana.
“Kazi kubwa zote kwa maana ya chanjo, kuweka pampu, sola,
vituo 11 vya kutolea maji sambamba na ujenzi wa tenki la lita elfu 90 juu ya
mnara wa mita 12 lipo kwenye hatua ya mwisho ya ukamilishaji-tunatarajia kukabidhi
mradi huu mapema Februari mwaka huu,” alisema Meneja Mkalimoto.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Ruwasa Wilaya ya Singida, Joel Kibusi, pamoja na
mambo mengine, alisema tayari wamepokea mabomba na vifaa vingine kwa ajili ya kuanza
kutekeleza mradi mwingine wa maji safi na salama ndani ya kijiji cha Mitula
ambao mpaka kukamilika kwake unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi milioni
316.
Kibusi akizungumza na wananchi wa kijiji hicho alisema hatua
ya kwanza kwa maana ya kupata chanjo kinachoweza kutosheleza mahitaji ya wakazi
hao imekamilika na mkandarasi tayari amepatikana na ujenzi unatarajia kuanza
ndani ya kipindi cha wiki mbili kuanzia sasa.
“Mradi wa Mitula utaanza kutekelezwa ndani ya wiki mbili
kuanzia sasa na utakamilika ndani ya miezi 2 mpaka mitatu. Kazi zitakazofanyika
ni pamoja na kujenga vituo 7 vya kuchotea maji ‘domestic points,’ tenki la maji
lenye ujazo wa lita elfu 75 litakalojengwa juu ya mnara wa mita 6, tutaweka
sola kisimani, ufungaji wa pampu mpya, uchimbaji na ulazaji mabomba na ujenzi
wa nyumba ya mashine,” alisema Kibusi.