Na Dotto Mwaibale, Singida.
SHIRIKA la Tanzania for Equal Opportunity (TAFEO) lenye makao yake makuu mkoani Singida linalojihusisha na kutengeneza urafiki na watu wanaoishi mazingira magumu wakiwepo Yatima kupitia Jumuiya ya Sant Egidio limegawa Rozari Takatifu, vifaa vya shule na chakula kwa Wakatoliki ambao wapo katika kundi la watu maalumu ili waweze kuzitumia kwa maombi mbalimbali.
Akizungumza jana wakati wa hafla ya kugawa msaada huo na rozari hizo iliyofanyika Ukumbi wa Social mjini hapa ambapo ipo ofisi ya shirika hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Stella Mwagowa alisema rozari hizo zimetolewa na Mary Maira ambaye ni mdau kutoka Kanisa Katoliki mkoani hapa ambaye ni mtengenezaji wa rozari hizo ambaye naye ana wadau ambao walimuunga mkono kuzitengeneza.
“Wadau hao walimuomba Maira baada ya kuzitengeneza rozari hizo zipelekwe kwa watu wanaoishi mazingira magumu kwa kupitia shirika hilo la TAFEO ambalo linafanya kazi zake kwa kushirikiana na jumuiya yake ya vijana wa vyuo wanao jitolea kupitia Sant Egidio” alisema Mwagowa.
Mwagowa alisema mbali ya kugawa rozari hizo pia shirika hilo lilimuunga mkono mdau huyo ambapo waliweza kugawa vifaa vya shule kama madaftari na kalamu kwa ajili ya wanafuzi ambao wataanza masomo yao Januari 17, 2022 ili ziweze kuwasaidia wakiwa shuleni.
Alisema pia walitoa mchele kwa watu wazima kwa ajili ya kusaidia makundi hayo hasa kwa wale wanaoishi majumbani na walezi wao.
Mwalimu Mary Maira akizungumza kwenye hafla hiyo alisema wadau waliomchangia na kuwezesha kutengeneza rozari hizo ni wanafunzi wake waliohitimu masomo yao ya kidato cha nne mwaka 2003 Shule ya Sekondari Paloti ambao walimtembelea nyumbani kwake na kumkuta akitengeneza rozari hizo na baada ya kuona ubunifu huo walimwezesha na kuzitengeneza rozari 40 na walielekeza rozari hizo zipelekwe kwa makundi hayo pamoja na Magereza.
“Tulishauriana na Mume wangu Benard Maira tuzilete rozari hizi katika shirika la TAFEO ili liweze kuzigawa kwa watu wenye mahitaji waweze kuzitumia kwa maombi mbalimbali kwani sala ya Rozari Takatifu hutoa nafasi ya kutafakari mafumbo ya maisha ya Yesu Kristu na Maria, katika safari ya wokovu wa mwanadamu” alisema Maira.
Mume wa Mary Benard Maira alitumia nafasi hiyo kuiomba jamii kuachana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, kama vile, ukeketaji, ubakaji na vingine vyote vinavyo husisha ukatili huo ambavyo havimpendezi Mungu.
Paroko wa Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Simion Gwanoga alisema anafarijika sana kwa mambo yanayofanywa na shirika hilo kwa kujitoa kusaidia watu wenye mahitaji na changamoto mbalimbali za kimaisha na kuwa jambo hilo si kwa mahitaji tu ya kimwili bali na roho katika imani.
Mwanafunzi Theresia Basila ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tano kutoka Katavi alilishukuru shirika hilo kwa kujitoa kwao kusaidia watu wenye changamoto mbalimbali na akayataka mashirika mengine kuiga mfano huo kwani unatoa faraja kwa walengwa.
“Niliombe shirika la TAFEO na mengine yabuni miradi midogo midogo ambayo itawahusisha vijana na makundi mengine ya watu wenye uhitaji ili waweze kujifunza kuiendesha jambo litakalo wasaidia kujikomboa kiuchumi badala ya kuwapata misaada hii ya kawaidia ambayo si endelevu” alisema Basila.