*************************
– Asema hayo wakati wa kupokea taarifa ya ripoti ya Kamati aliyounda kuchunguza Migogoro sugu Ya Ardhi Mabwepande.
– Aelekeza Vyombo vya dola kuwakamata vinara waliosababisha Migogoro hiyo.
– Akabidhi ripoti kwa DC Gondwe na kumuelekeza kufanyia kazi Mapendekezo yote 19 ya Kamati.
– Asema atakabidhi taarifa hiyo pia kwa Waziri wa Ardhi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla leo January 05 amepokea ripoti ya Kamati aliyounda kuchunguza Migogoro sugu ya Ardhi eneo la Mabwepande ambapo Kamati hiyo imetoa Mapendekezo 19 ya kufanyia kazi kumaliza Mgogoro huo.
Akipokea ripoti hiyo RC Makalla ameikabidhi ripoti kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe na Mkurugenzi wa Kinondoni na kuwaelekeza kuhitisha kikao Cha Kamati ya Ulinzi na usalama Wilaya ili kupitia ripoti na kutekeleza Mapendekezo 19 ya Kamati.
Aidha RC Makalla ameelekeza Vyombo vya dola kuwakamata watu wote waliobainishwa na Kamati kuwa vinara wa kusababisha Migogoro na kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa.
Hata hivyo RC Makalla amesema ripoti hiyo ataikabidhi pia kwa Waziri wa Ardhi huku akielekeza Watuhumiwa wote ambao wapo Chini ya Mamlaka ya Chama Cha Mapinduzi CCM kufikishwa kwenye Kamati ya maadili na kuchukukiwa hatua.
Pamoja na hayo RC Makalla amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Godwin Gondwe kumpatia Mpango kazi wa kutekeleza Mapendekezo yote 19 ya Kamati na kuipongeza Kamati kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Siraji Ngarambe amesema Kamati hiyo ilifanya kazi kwa muda wa siku 78 na wamebaini miongoni mwa sababu za Migogoro walizobaini Ni pamoja na Watendaji wa Kata, Mitaa, Wajumbe wa shina wasio waaminifu, ugawaji wa Maeneo pasipo kufuata taratibu, Rushwa, matumizi mabaya ya kauli za Viongozi, dhana iliyojengeka kwa baadhi ya Wananchi kuvamia maeneo ili walipe fidia na nyinginezo.