Waziri wa Nchi ,Afisi ya Makamo wa Pili wa Raisi ,Sera,Uratibu na Baraza la Wawakilishi Dkt.Khalid Salum Mohammed akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mradi wa uvivu wa Bahari Kuu ,huko Makao Makuu ya Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) Kibweni Zanzibar.
…………………………………………..
Na Rahima Mohamed ,Maelezo
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuweka miundombinu rafiki ya kuhifadhi samaki na bidhaa zinazopatikana baharini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,Sera,Uratibu na Baraza la Wawakilishi Khalid Salum Mohamed wakati akizindua mradi wa uvuvi wa bahari kuu huko makao makuu ya Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM)Kibweni Mkoa wa Mjini Magharib ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 58 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Amesema ni lazima tutumie rasilimali ya bahari katika kukuza uchumi pamoja na kutengeneza mazingira mazuri kwa watumiaji ili kupata soko la ndani na nje ya nchi.
Waziri Khalid amekipongeza kikosi hicho kwa uamuzi wao wa kuwekeza katika uvuvi wa bahari kuu kwa lengo la kujijengea wenyewe kiuchumi na kusaidia serikali kufikia azma Uchumi wa Buluu.
Aidha amewataka kutumia ipasavyo bahari katika ukulima wa mwani, ufugaji wa samaki na majongoo bahari ili kuinua kipato cha wananchi na taifa kwa ujumla.
Nae mkuu wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) Commodore Azana Hassan Msingiri ameiomba serikali kuwapatia kifaa maalum cha kuchunguza samaki waliopigwa na mabomu ambacho kitasaidia kudhibiti uvuvi haramu nchini.
Akitoa wito kwa wananchi amewataka kuachana na uvuvi haramu ili mazalio ya samaki yahifadhiwe ili kuiunga mkono serikali kufikia lengo lake la Uchumi wa Buluu.