Muongoza watalii abdalah akionesha moja ya magofu ya kale yanayopatikana katika kisiwa cha Songomnara wilaya Kilwa mkoani Lindi, ambayo yanayosimamiwa na Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania TAWA.
Muonekano wa viombe vya baharini ikiwa ni moja ya kivutio kinachopatikana katika visiwa vya Kilwa Kisiwani na Songomnara wilaya Kilwa mkoani Lindi.
***********************
NA FARIDA SAIDY, KILWA.
Wananchi wilayani Kilwa mkoani Lindi, wametakiwa kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii kufuatia uamuzi wa dhati uliyochukuliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kufungua milango kwa kutangaza vivutio vinavyopatikana katika wilaya hiyo.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mkuu wa wilaya hiyo Bi. Zainabu Kawawa, ambapo amesema TAWA inafanya kazi kubwa ya kutangaza utalii wa kusini hususan unaopatikana katika wilaya ya Kilwa.
Ameongeza kuwa pamoja na kazi kubwa inayofanywa na TAWA ya kutangaza vivutio vya utalii vinavyowavutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi. mamlaka hiyo imeweka mazingira rafiki kwa watalii kwa kununua boti ya kisasa.
Mkuu huyo wa wilaya amesema, boti hiyo ina uwezo wa kusafirisha watalii kutoka kisiwa kimoja hadi kingine, huku wakifurahia kuangalia viumbe mbalimbali wa majini wakiwa ndani ya boti hiyo.
Amesema utalii wa majini unaopatikana katika visiwa vya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara, ni pamoja na utalii wa Matumbawe, ambao watalii wanaweza kuona viumbe vya chini ya bahari kupitia boti ya kisasa iliyonunuliwa na TAWA.
Vivutio vingine ni utajiri mkubwa wa historia kupitia malikale (magofu), ambao kwa upekee wake, umeingizwa katika orodha ya urithi wa dunia, inayotambuliwa kimataifa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
“Mbali na magofu yanayopatikana, pia mtalii anapopata fursa ya kutembelea visiwa hivyo atapata muda wa kufahamu historia nzima ya mji wa Kilwa na uzuri wake, tangu karne ya 13 pamoja na kufurahia upepo wa Pwani kutoka bahari ya Hindi,” amesema.
Kwa upande wake Samson Gisiri, Mhifadhi kutoka TAWA, ambao wamepewa dhamana ya kusimamia malikale, alisema moja kati ya kazi ya mamlaka hiyo ni kusimamia na kutunza malikale zilizopo katika visiwa vya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.
Aidha, ameongeza kuwa katika kuweka mazingira rafiki kwa watalii, TAWA imeanza kujenga sehemu maalumu za malazi kwa ajili ya watalii Kilwa Kisiwani, ili kuwafanya wafurahie muda wao katika visiwa hivyo.
Mhifadhi huyo amewataka Watanzania kutembelea maeneo ya Songo Mnara na Kilwa Kisiwani, ili kujionea urithi wa dunia unaopatikana katika visiwa hivyo.