Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Songea mjini Dkt Damas Ndumbaro katikati akiwaongoza baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Songea kutembelea Bustani ya Wanyama ya Luhira Zoo iliyopo kata ya Msamala Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,kushoto ni Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Michael Mbano.
Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea mjini Dkt Damas Ndumbaro katikati akimsikiliza mkazi wa Manispaa ya Songea ambaye hakufahamika jina lake,wakati wa Tamasha la kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika Bustani ya Wanyama ya Luhira iliyopo kata ya Msamala Manispaa ya Songea,kushoto kwa Waziri Ndumbaro ni mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Michael Mbano.
aadhi ya wakazi wa WAdau wa Utalii Masumbuko Mbogoro katikati na aliyejitambulisha kwa jina moja la Kudeka kulia,wakifurahia jambo na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro aliyevaa kapero,wakati wa Tamasha la kutembelea na kutangaza vivutio vya utalii katika Bustani ya Wanyama ya Luhira Zoo iliyopo kata ya Msamala Manispaa ya Songea.
Picha zote na Muhidin Amri
………………………………………………………………………..
Na Muhidin Amri,Songea
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro,amewaongoza wakazi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kushiriki Tamasha la Utalii na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii katika Bustani ya Wanyama ya Luhira iliyopo kata ya Msamala Manispaa ya Songea.
Katika Tamasha hilo lilihudhuriwa na mamia ya Wa kazi wa Manispaa ya Songea na wale wanaotoka wilaya jirani ya Namtumbo na Mbinga ,lilipambwa na Ngoma,vyakula vya asili,nyama choma pamoja na vinywaji.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika Tamasha hilo Kamanda wa Uhifadhi wa Wanyamapori(Tawa)Kanda ya Kusini Abraham Jullu, amewataka Watanzania hususani wakazi wa mkoa wa Ruvuma kujenga tabia ya kufanya utalii wa ndani ili kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo katika mkoa wao.
Alisema,lengo la Tamasha hilo ni kuhamasisha utalii wa ndani kwa wakazi wa mkoa wa Ruvuma uliobarikiwa kuwa na utajiri wa vivutio vingi ambavyo bado havijafahamika sana kwa wenyeji wa mkoa huo.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro,amewataka wananchi wa mkoa wa Ruvuma ni mikoa ya Nyanda za juu na Kusini mwa Tanzania kwenda kufanya utalii katika Bustani ya Luhira ambayo ina upekee kutokana na wanyama na vivutio vingine vilivyopo.
Dkt Ndumbaro ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini ametaja wanyama wanaopatikana katika Bustani hiyo ni Pofu,Pundamilia,Swalapara,Kudu,Mamba wakubwa,Chatu.
Dkt Ndumbaro alisema, mpango wa baadaye ni kuongeza wanyama wengi zaidi katika Bustani hiyo ambao watashawishi wananchi kufanya utalii wa mara kwa mara na Serikali kupata mapato.
Aidha,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kuimarisha sekta ya Utalii hapa nchini ikiwemo kutoa fedha kupitia mpango wa maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Covid-19 ambazo zimesaidia kuboresha utendaji kazi wa wa sekta ya utalii na wizara hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho,ameipongeza Wizara hiyo kwa kazi nzuri na ilivyojipanga vyema kuleta mabadiliko makubwa kwenye suala la utalii wa ndani.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano,amewaomba wakazi wa ndani na nje ya Manispaa ya Songea kutumia fursa ya uwepo wa Bustani ya Wanyama Luhira kwenda kutembelea na kuona vivutio vingi vilivyopo ambavyo ni urithi wa wana Songea na Watanzania kwa jumla.
Mbano ambaye ni Diwani wa kata ya Msamala alisema,wakazi wa mkoa wa Ruvuma wana kila sababu ya kujivunia kuwepo kwa Bustani ya Wanyama Luhira, ambavyo vitakuwa moja kati ya vyanzo vikubwa vya mapato na baadhi ya watu watapata ajira na hivyo kuinua uchumi wao na Manispaa ya Songea.