WAZIRI wa Viwanda na Biashara Prof.Kitila Mkumbo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Januari 4,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya kuongeza muda wa kuwasilisha taarifa za wamiliki manufaa wa Kampuni (Beneficial Owners).Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Godfrey Nyaisa
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Prof.Kitila Mkumbo, akitoa taarifa ya kuongeza muda wa kuwasilisha taarifa za wamiliki manufaa wa Kampuni (Beneficial Owners) leo Januari 4,2022 jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Biashara na Viwanda Bw.Christopher Mramba,akimkaribisha Waziri wa Viwanda na Biashara Prof.Kitila Mkumbo,kutoa taarifa ya kuongeza muda wa kuwasilisha taarifa za wamiliki manufaa wa Kampuni (Beneficial Owners) leo Januari 4,2022 jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Makampuni na Majina ya biashara kutoka Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),Meinrad Rweyamamu,akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) waliouliza maswali katika Mkutano wa Waziri wa Viwanda na Biashara Prof.Kitila Mkumbo, leo Januari 4,2022 jijini Dodoma.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Godfrey Nyaisa ,akijibu Maswali ya waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Mkutano wa Waziri wa Viwanda na Biashara Prof.Kitila Mkumbo, leo Januari 4,2022 jijini Dodoma.
…………………………………………
Na Alex Sonna, Dodoma
Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof.Kitila Mkumbo, ameongeza muda wa miezi sita kwa kampuni kuwasilisha taarifa za wamiliki manufaa wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
Hata hivyo, amesema kwa kampuni zitakazoshindwa kuwasilisha hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Prof.Mkumbo ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu kuongeza muda wa miezi sita kwa ajili ya kuwasilishwa taarifa hizo.
Amesema awali taarifa hizo zilipaswa kuwa zimewasilishwa ifikapo Desemba 31, mwaka jana lakini kutokana na maombi ya wawekezaji kuhusu kuongeza muda, hivyo serikali imeongeza miezi sita ili kutoa nafasi kwa wamiliki hao kuwasilisha taarifa zao.
Waziri huyo amesema kampuni zilizowasilisha taarifa hizo hadi jana ni 14,026 sawa asilimia 14 ya matarajio.
Amefafanua kuwa kampuni zote nchini husajiliwa na BRELA na hupaswa kutoa taarifa kadhaa ikiwamo wamiliki manufaa wa kampuni na awali hazikulazimika kisheria kutoa taarifa za waliopo nyuma ya kampuni(wamiliki manufaa) lakini kwasasa ni lazima.
“Hawa wamiliki manufaa ndio wenye mtaji na wanaendesha kampuni, hivyo Benki ya Dunia na taasisi zingine kimataifa zimehimiza kueleza kwa uwazi umiliki wa kampuni,”amesema.
Amesema kutokana na umuhimu wa taarifa hizo na kwa mamlaka aliyonayo kisheria ameongeza muda huo hadi Juni 30, mwaka huu ili wamiliki wote watimize matakwa ya sheria.
“Niwahimize wamiliki wote watumie muda vizuri wa nyongeza na sheria ipo wazi kwa yule ambaye hatawasilisha taarifa zake hatua gani zitachukuliwa dhidi yake,katika kujenga mahusiano mema na wafanyabiashara tumekubaliana kuongeza muda huu,”amesema.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Makampuni na Majina ya biashara kutoka BRELA,Meinrad Rweyamamu, amesema sheria ya makampuni imeweka utaratibu pale ambapo mtu atachelewesha kuwasilisha taarifa atakumbana na adhabu ya kulipa Sh.2500 kila mwezi.
“Kwa kila mwezi ambao atakuwa amechelewesha taarifa atapaswa kulipa kiasi hicho, sambamba na hilo ikibainika haikuwasilisha taarifa za wamiliki manufaa au kuwasilisha taarifa ambazo si za kweli Mahakama itaipiga adhabu kampuni hiyo ya faini kuanzia Sh.Milioni tano hadi 10,”amesema.
Amesema kampuni ambazo zimekuwa zikipeleka taarifa za mwaka ni zaidi ya 140,000 na kwamba bado kampuni nyingi hazipeleki taarifa zao BRELA hivyo wanatarajia kutoa taarifa ya kampuni zisizo hai ili zihuishe taarifa zao.