Katibu mkuu wizara ya Afya, maendeleo ya jamii ,wazee ,jinsia na watoto idara kuu ya maendeleo ya jamii,Dokta John Jingu akizungumza katika mkutano huu jijini Arusha leo.
**********************
Happy Lazaro, Arusha
Arusha.Serikali imesema iko katika hatua za mwisho za mchakato wa kukamilisha uundwaji wa Baraza la Wazee Kitaifa ambalo litakuwa sauti ya wazee katika ngazi ya Taifa.
Aidha imeweza kudhibiti kwa kiwango kikubwa mauaji ya wazee yaliyokuwa yakifanyika katika miaka nyuma ambayo yalikuwa yakihusisha masuala ya imani za kishirikina.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Wazee,Jinsia na Watoto -Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii,Dk.John Jingu,akizungumza ma wawakilishi wa mabaraza ya wazee mkoa wa Arusha,viongozi wa mila na Maafisa ustawi wa jamii kutoka halmashauri zilizopo mkoani hapa.
Amesema kuwa serikali inawajali wazee kwani ni nguzo muhimu katika jamii hivyo moja ya masuala inayofanya ni kumalizia mchakato wa kukamilisha uundwaji wa baraza la wazee kitaifa ambalo litakuwa sauti ya wazee.
“Lingine ambalo serikali imeweza kufanya ni kudhibiti kwa kiwango kikubwa mauaji ya wazee ambayo huko nyuma yalikuwa yakifanyika huku wengine wakihusisha na masuala ya imani za kishirikina,”amesema
“Serikali inafanya jitihada nyingi kulinda na kukuza ustawi wa wazee,inawathamini kwani ni nguzo muhimu kwa jamii na ndiyo maana tumekutana leo tubadilishane mawazo na kuangalia sisi kama serikali tunatimiza vipi wajibu wetu kwa kundi hili muhimu,”
Akitoa taarifa ya utoaji huduma kwa wazee mkoa wa Arusha kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba 2021,Afisa Ustawi wa Jamii mkoani hapa,Dennis Mgiye,amesema mkoa umeitikia wito wa kutambua wazee ambapo wameweza kutambua wazee 67,497 ukilinganisha na wazee 64,999 waliotambuliwa mwaka 2020.
“Mkoa umeendelea kuwapatia wazee vitambulisho ambapo hadi sasa wazee 37,262 sawa na asilimia 56 wamefikiwa na tumeazimia ifikapo Juni mwaka huu,kila halmashauri iwe imekamilisha zoezi hilo na hadi Desemba mwaka jana mabaraza 688 yameundwa kuanzia ngazi za vijiji/mitaa katika mkoa wetu,”amesema
Ametaja changamoto zinazokabili kada hiyo ni pamoja na uchache wa Maafisa Ustawi wa jamii kwenye ngazi za halmashauri hasa kata na vijiji huku wilaya ya Longido ikiwa na Afisa Ustawi wa jamii mmoja tu.
Mwakilishi wa baraza la wazee mkoa wa Arusha,Khamis Ramadhan,ameomba serikali kukamilisha mchakato wa Sheria ya Wazee kwani tangu kuundwa kwa Sera ya wazee mwaka 2003 hadi sasa hakuna sheria inayosimamia sera hiyo.
“Ni miaka 19 tangu kutungwa kwa sera hiyo ila hadi sasa sheria bado tunaomba sheria ya wazee iwepo ili iweze kusimamia sera hii na iweze kuendana na wakati,”amesema na kuongeza
“Changamoto nyingine ni kukosekana kwa bajeti ya mabaraza ya wazee,hii inasababisha tunashindwa kutekeleza majukumu yetu ipasavyo,”