Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt John Jingu akizungumza na Wazee wa Mkoa wa Arusha katika kikao kilichomkutanisha na Baraza la Wazee la Mkoa huo.Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Arusha Mhina Sazua akielezea changamoto zinazowakabili mbele ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu katika kikao kilichowakutanisha na Baraza la Wazee la Mkoa huo. Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Dkt. Athuman Kihemia akielezea Jinsia Mkoa huo unavyoyalea Mabaraza ya Wazee Mkoani humo katika kuhakikisha wanapata muda wa kukutana na kuzungumza masuala yao katika kikao kilichoikutanisha Wizara na Baraza la Wazee la Mkoa. Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii Tullo Masanja akielezea namna Wizara inavyoshirkiana na Mikoa na Wilaya katika Kuratibu Uanzishwaji wa Mabaraza ya Wazee katika kikao kilichoikutanisha Wizara na Baraza la Wazee la Mkoa wa Arusha. Baadhi ya Wazee wa Mkoa wa Arusha wakimsikiliza (hayupo pichani) wakati wa kikao kilichowakutanisha Wizara na Baraza la Wazee la Mkoa.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu katika picha ya pamoja na Wazee wa Baraza la Wazee Mkoa wa Arusha akiwemo mzee wa Kimila Laigwanan Tobiko mara baada ya kikao kilichofanyika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa. Kulia kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Dkt. Athuman Kihemia na kushoto kwake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee mkoa wa Arusha Mzee Mhina Sazua.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WAMJW
********************
Na Mwandishi Maalum, Arusha
Serikali imesema inaandaa kazi data ya Wazee wenye ujuzi katika fani mbalimbali kwa lengo la kuwalea Vijana wataalam wapya katika Sekta mbalimbali ili kuwapa uzoefu na mbinu za kufanya kazi kwa ufanisi.
Hayo yamesemwa Mkoani Arusha na Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu wakati akizungumza na Baraza la Wazee Mkoani humo.
Amesema Wazee waliofanya kazi katika Sekta mbalimbali kupitia Mabaraza ya Wazee katika ngazi za Mikoa na Halmashauri watakuwa na mchango mkubwa wa kuwarithisha wataalam vijana uzoefu na ujuzi na mbinu za kufanikisha utendaji ili kuwawezesha kufanya kazi kwa weledi na uzalendo.
“Nitoe wito kwa Wazee, haya Mabaraza yanaweza kutambua ujuzi wa wazee mbalimbali hivyo tutatumie vizuri katika kuhakikisha vijana wanaochipukia katika Sekta mbalimbali wanapata uzoefu wa Wazee katika Sekta hizo” alisema Dkt. Jingu
Aidha, ameongeza kuwa Serikali inaendelea na jitahada kuwalinda Wazee dhidi ya vitendo vya ukatili kwa kutekeleza Mpango wa Kutokomeza Mauaji ya Wazee wa Mwaka 2018/2019- 2022/2023 ambao unalenga katika kushirikiana na wadau katika kuwalinda Wazee na vitendo hivyo.
“Serikali itaendelea kuhakikisha Wazee wanalindwa na vitendo vya ukatili na kupata huduma nzuri za Afya katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na uzee” alisema Dkt. Jingu
Pia Dkt. Jingu amesema Mabaraza ya Wazee yanaweza kuwa fursa ya kufanya shughuli za kiuchumi kwa kuwakutamisha Wazee wenye uelekeo mmoja katika Sekta fulani ili waweze kujitegemea zaidi.
Pia amewaomba Wazee kukemea mambo ambayo hayaendani na Mila na desturi za Mtanzania katika maeneo yao ili kuwa na kizazi chenye maadili mema uzalendo na upendo kwa nchi yao.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Dkt. Athumani Kihemia amesema Mkoa umeweka jitihada za kuhakikisha katika kusimamia maagizo ya Serikali hasa katika kuziagiza Halmashauri kutenga Bajeti kwaajili ya kuratibu masuala ya Wazee aktika maeneo yao.
Pia amewataka watendaji wa Serikali hasa Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuendelea kusimamia masuala ya Wazee na kuhakikisha Wazee wanapata huduma stahiki na hasa huduma za Afya.
Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Wazee Mkoa wa Arusha Mzee Hamis Ramadhan akisoma risala ya Wazee wa Mkoa wa Arusha ameiomba Serikali kuboresha Sera ya Wazee itakayoendana na wakati na kuyajengea uwezo wa Mabaraza ya Wazee nchini ili kuyapa uwezo wa kuratibu masuala ya Wazee kwa Ustawi wao.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Arusha Denis Mgiye akitoa taarifa ya mkoa amesema kuwa Mkoa unapata changamoto ya kuratibu na kusimamia masuala ya Wazee kutokana na upungufu wa Maafisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri, uchache wa wadau katika eneo la Wazee na ufinyu wa Bajeti katika masuala ya Wazee na huduma za Ustawi wa Jamii.