****************
Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa sura ya 290 kifungu cha 37A(1-4) kinaeleza kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zitatenga asilimia kumi (10%) ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwezesha vikundi vilivyosajiliwa vya wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.
Katika kutekeleza hilo, kwa robo ya pili Oktoba-Desemba 2021/22, Halmashauri ya Wilaya ya Muleba imetoa mkopo wa fedha Tsh. milioni 558.63 kwa vikundi 70 vya Akina Mama, vikundi 15 vya Vijana na vikundi 10 vya Watu wenye Ulemavu.
Akizungumza katika shughuli hiyo Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila amewasihi vikundi vilivyopokea mkopo huo, kuzitumia fedha zilizotolewa zikafanye kazi iliyopangwa kama ambavyo wameelimishwa na wataalamu kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii na maafisa kutoka benki ikiwa ni pamoja na kukuza mitaji na biashara zao.
“Serikali iliona uhitaji wa kuwezesha jamii ikaamua kutoa mikopo isiyokuwa na riba. Mikopo hii mliyokopeshwa mtaanza kurejesha baada ya siku 90 yani miezi mitatu hivyo nawasihi fedha hii mliyokopeshwa muende kufanyia biashara na shughuli za ujasiriamali iwe ni ufugaji, iwe ni uvuvi ama ufundi na shughuli zingine za kimaendeleo ili muinue vipato vyenu na kukuza uchumi wa Taifa letu. Mwende mkafanye biashara msiende kuifanyia matumizi mengine yasiyo ya manufaa,” amesema na kusisitiza Mhe. Nguvila.
Pia amewahasa kuzitumia fedha hizo kuwatoa kwenye hali ya chini kwenda kwenye hali ya kati na hata ya juu ya kiuchumi lakini pia amewasisitiza kutozitumia fedha hizo kwa ajili ya kununua nguo bali itumike kuinua hali zao za kimaisha na kuwaletea maendeleo.
Aidha, amewaomba vikundi hivyo kuhakikisha wanakuwa waaminifu sana katika suala la kurejesha fedha hizo ambapo amewasihi kutokuanza kusubiri wataalamu wa maendeleo ya jamii kuwafuatilia bali wao wenyewe wakumbushane kurejesha hizo fedha ili ziweze kutumika kuwakopesha na watu wengine.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba Ndg. Elias Kayandabila ameviomba vikundi vilivyopokea mikopo hiyo kuhakikisha wanakwenda kuzitumia fedha zile kufanya yale ambayo wamekubaliana na ambayo wameelekezwa kwenye mafunzo yaliyotolewa na watu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba Mhe. Magongo Justus amevisihi vikundi vya Akina Mama, Vijana na Watu wenye Ulemavu kuhakikisha wanazitumia vizuri fedha hizo ili waweze kupata faida ili ile faida ambayo wangerejesha kama riba basi ndio iwasaidie kununua mboga na hata kuwasaidia kufanya shughuli nyingine ambazo wanafikiri wangezifanya lakini kwanza wazalishe kwa mujibu wa malengo ya mikopo waliyopewa.
Mbunge wa jimbo la Muleba Kusini Mhe. Dr Oscar Kikoyo amevisisitiza vikundi hivyo kuwa hiyo fedha iliyotolewa kwao ni fedha ya mzunguko, wamekopeshwa wakizalisha robo ya tatu vitakopeshwa vikundi vingine hivyo amewaomba wazitumie fedha hizo kuzungusha katika biashara zao na kuhakikisha wanarejesha ili robo ya tatu Januari-Machi, 2021/22 waweze kukopeshwa vikundi vingine.
Jovitha Juston ambae ni miongoni mwa wanakikundi waliopokea mkopo, pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji wanawake kiuchumi wilaya ya Muleba amemshukuru sana Mhe. Samia Suluhu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwezesha jamii kwa mikopo hii isiyokuwa na riba inayowawezesha makundi haya kuinuka kiuchumi na hata kumudu maisha yao ya kila siku.
Kwa upande wao wananchi ambao ni wanavikundi vilivyopokea mikopo hiyo katika nyakati tofauti wametoa pongezi na shukrani zao kwa uongozi wa Serikali ya awamu ya sita na Halmashauri ya wilaya ya Muleba kwa utoaji wa mikopo ambayo haina riba. Wamesisitiza kuwa fedha hizo watazifanyia kazi iliyokusudiwa kama inavyostahili na kuzirejesha fedha hizo kwa wakati.
Imetolewa na:
Kitengo cha Teknolojia ya Habari, Mawasiliano na Uhusiano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.