********************
Na. WAMJW – KILIMANJARO
Chanjo ni kinga dhidi ya magonjwa inayosaidia kuzuia milipuko ya magonjwa, ulemavu wa kudumu ambao hupelekea madhara ya kiuchumi, kijamii na vifo.
Hayo yamesemwa leo na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Credianus Mgimba kwenye mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Kilimanjaro,Tanga na Manyara kuhusu chanjo ya UVIKO-19 yaliyofanyika Mkoani Kilimanjaro.
Dkt.Mgimba amesema Wizara ya Afya inatoa kipaumbele kwa huduma za kinga ikiwemo kutoa chanjo zote muhimu kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano na akina mama wajawazito.
Kwa sasa Wizara ya Afya inaendelea kutoa chanjo kwa wasichana wa umri wa miaka 14 dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi na kutoa chanjo za UVIKO-19 kwa watu wente umri kuanzia miaka 18 na kuendelea
“Chanjo zinazotolewa kwa watoto chini ya miaka mitano ni pamoja na zile za kukinga magonjwa ya polio, kifua kikuu, pepo punda, kifaduro, dondakoo,homa ya ini, homa ya uti wa mgongo, nimonia, kuhara, surua pamoja na Rubella.”amesema Dkt. Mgimba
Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya juhudi za kuboresha huduma kwa kuongeza vituo vingi vya Afya vinavyotoa huduma za chanjo hadi kufikia 7000 kwa nchi nzima.
“Niwahakikishie wananchi kuwa chanjo zinazotolewa katika vituo vyetu ni salama, hutolewa na wataalamu wenye uzoefu Mkubwa na waliobobea katika fani hii kwa muda mrefu na hutolewa bure bila malipo.” Amesema Dkt. Mgimba
Kwa upande wake Afisa Programu-Mpango wa Taifa wa chanjo Dkt.Georgina Joachim amewasihi waandishi wa Habari kuendelea kutoa elimu juu ya kupata chanjo zote zinazotolewa dhidi ya UVIKO 19 bila kuchoka.
“Chanjo ni hiyari lakini lazıma tuambizane ukweli juu ya umuhimu wa chanjo hizi zinasaidia sana ni muhimu kuendelea kuchanja na chanjo zinapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya.”amesema Dkt .Joachim
Aidha,Mratibu wa chanjo Mkoa-Kilimanjaro Peter Kihamia amesema Mkoa wa Kilimanjaro umekuwa na hamasa kubwa kwa wananchi kujitokeza kupata chanjo ukilinganisha na mikoa mengine hii imetokana na mshikamano kwa viongozi wa Mkoa.
“Tunahitaji nguvu kwa pamoja ili tufikie lengo kwa wananchi kupata chanjo muhimu zinazotolewa katika sehemu zote zinazotoa huduma hii ya chanjo dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO-19.” amesema Kihamia