**********************
MICHUANO ya Mpira wa Miguu maarufu kama Mwenda Cup yamehitishwa rasmi Mikocheni kwa timu ya Wanyama Fc ya kuibuka na ushindi baada ya kuibwaga timu ya Mkunguni Fc kwa mikwaju ya penati.
Fainali hiyo ya vuta nikuvute huku timu zote zikionyeshana ufundi, ilishuhudiwa dakika tisini za mchezo zikimalizika kwa timu zote bila kufungana hivyo kulazimu kupigwa penati ili kumpata mshindi.
Hata hivyo ni timu ya Wanyama ndiyo iliibuka kuwa mbabe dhidi ya mwenzake baada kipa wake kudaka mikwaju miwili ya penati kati ya mitano iliyopigwa huku wenzao wakipata yote hivyo kuwafanya waibuke ushindi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam Kate Kamba, ndiye aliyekabidhi kombe kwa mshindi huyo sambamba na zawadi ya Pikipiki.
Timu ya Mkunguni iliibuka kuwa mshindi wa pili na kukabidhiwa kiasi cha Shilingi Milioni Moja na mpira, wakikabidhiwa zawadi hiyo kwa niaba ya michuano hiyo na Meya wa Kinondoni Songoro Mnyonge.
Mshindi wa tatu wa michuano hiyo ya Mwenda Cup iliyodhaminiwa na Taasisi ya Mwenda Foundation ilikwenda kwa timu ya Huruma siyo Malezi, ambayo iliifunga timu ya ‘Master Plan’ 1-0 na kupata kiasi cha Shilingi Laki tano na mpira iliyokabidhiwa na Mbunge wa Kinondoni Abbas Tarimba.
Timu ya ‘Master Plan’ walifanikiwa kuwa washindi wa nne na kukabidhiwa kiasi cha Shilingi Laki Tatu na mpira, zawadi iliyokabidhiwa na Mdhamini wa michuano hiyo kupitia taasisi ya Mwenda Foundation Yusuf Mwenda.
Mbali hizo, michuano hiyo ilishuhudiwa pia makundi mbalimbali yakiibuka na zawadi ya fedha zilitolewa kwa kipa bora pamoja na washangiliaji bora huku fainali hiyo ikishuhudiwa kuwavutia mamia ya mashabiki waliofurika katika uwanja wa Shule ya Msingi ya mikocheni ‘A’
Jumla ya timu 16 zilishiriki michuano hiyo iliyoanza Desemba 17 lengo lake kuu ni kuhamasisha ujirani mwema, undugu na urafiki baina ya wachezaji pamoja na mashabiki.