…………………………………………..
Adeladius Makwega,Dodoma.
Kati ya mwaka 1996-1998 niliwahi kuishi eneo la Ndanda ambapo huko nilikwenda kama mwanafunzi wa kidato cha tano na kuhitimu kidato cha sita. Nilipofika hapo kama mwanafunzi wa masomo ya Historia, Kiswahili na Kiingereza nilikutana na simulizi tatu za mambo makubwa ambayo yalisimuliwa sana na wanavijiji wa eneo hilo.
Kwanza mafuriko yaliyotokea nyuma ya miaka hiyo na kusabisha vifo vya watu katika eneo hilo, huku bweni la wanafunzi wa Ndanda kubomolewa na mafuriko na ndipo Wamishonari wa Benediktini wa Ndanda walipoamua kuwajengea bweni lengine wanafunzi wa kike wa Ndanda sekondari, Pili ni kifo cha Mwandishi wa Habari wa Rais Ali Hassani Mwinyi, marehemu Habibu Halahala aliyefariki kwa ajali ya Bangaboi akiwa katika maeneo hayo na jambo la tatu ni ujio wa Wazungu katika Kijiji cha Chiwata.
Mwanakwetu Mungu akinijalia nitakusimulia mada zote hizo tatu lakini leo nakusimulia juu ya mada moja yaani juu ya Kijiji cha Chiwata na ujio huo wa wazungu. Nikiwa mwanafunzi wa Ndanda mwalimu mmoja ambaye alikuwa akitwa Mtauka niliwahi kukusimulia katika matini yangu ya bundi mwenye maandishi ya kiarabu, mwalimu huyu alikuwa ni mkali sana huku akisimamia nidhamu ya wanafunzi.
Mwalimu huyu alikuwa kila mara akisimama mstarini alikuwa akilitaja neno KULOMBA. Jambo hilo lilinipa hamsa ya kuwauliza wanafunzi wezangu wenye asili ya huko maana yake, waliniambia kuwa Kulomba ni neno la kabila la Kiyao linalomaanisha mahusiano ya kimapenzi /Kuoa.
Neno hilo lilikuwa ni miongoni mwa maneno yangu ya kwanza kuyafahamu kwa Kiyao ambalo nimeyahifadhi katika kumbukumbu zangu za wakati huo. Nikiwa shuleni hapo nilipokuwa nikipata upenyo wa kutoka shuleni, tulikuwa tukitembelea vijiji jirani na Ndanda angalau kujifunza mambo mengi likiwamo hata la ulaji wa panya. Ambalo kwangu lilikuwa jambo geni. Huku nikiwaonja panya hao waliokausha vizuri kwa kuwekewa miti katikati na kubanikwa kando ya moto, wakiuzwa katika vilabu vingi vya pombe.
Nilijaribu kula panya hao niliona ni nyama nzuri na tamu ambayo haikuwa na shida yoyote ile na pengine Mungu akinijalia nikipa wasaa wa kufika Masasi lazima nitawatafuta panya hao niwale.
Tabia hiyo ya kukata mbuga ililinipeleka hadi katika Kijiji cha Chiwata ambapo kulikuwapo na rafiki yangu mmoja aliyekuwa mzaliwa wa hapo. Kwa yule ambaye haifahamu Masasi vizuri Kijiji cha Chiwata kipo umbali wa karibu wa Kilomita 20 na ushehe kutoka Masasi Mjini. Kijiji hichi kinajishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara.
Inaaminika kuwa Wamisionari wa Shirika la UMCA walifika Masasi na waliweka kambi yao katika eneo linalofahamika kama Mtandi ambalo hapo awali eneo hilo lilifahamika kama Kwitonji umbali wa Kilomita kama nane kutokea Masasi Mjini. Wamisionari hao walipokaa hapo walibaini kuwa eneo hilo halina maji ya kutosha kwa hiyo walihamishia makaazi yao Mkomaindo. Huku wengine wakibaki huko huko Mtandi.
Wakiwa hapo Wamisionari hao waliona kuwa suala la maji bado lilikuwa ni shida kwa hiyo waliamua kuwauliza wenyeji eneo lingine lenye maji ya kutosha ili waweze kuweka makaazi yao, hapo ndipo walipojulishwa kuwa kuna eneo linalofahamika kama KUVATAMA.
Kama ilivyokuwa desturi ya Wamisionari walipofika hapo walijenga zahanati na taasisi kadhaa za dini hiyo. Hizo taasisi zilikuwa zikitoa huduma kadhaa kwa wananchi wa hapo na maeneo jirani. Hasa hasa kupata huduma za tiba na hilo likavutia ujio wa watu wengi kwenda KUVATAMA kupata tiba katika zahanati iliyojengwa ikifahamika kama Zahanati ya Chidya.
“Jamani vipi huko mnakwenda wapi? Walijibu kuwa tunakwenda Kuvatama.” Kila siku iliyokuwa ikienda kwa Mungu watu walimiminika. Sasa watu waliokuwa wakitoka katika makabila mengine ambao si Wayao nao walikuwa miongoni mwa wapata huduma hiyo ya afya. Watu hao wa makabila mengine walishindwa kusema KUVATAMA bali walisema KUWATAMA.
Siku zilipozidi kusonga neno hilo lilionekana na refu mno ndipo watu wenyewe wakalifupisha kuwa KUWATA na wakaondoa silabi MA. Maisha yaliendelea na baadaye wakaondoa Silabi KU na kuwa CHI kulingana na matamshi yao , hapo ndip eneo hilo likaitwa CHIWATA.
Hadi leo hii eneo hilo linaitwa CHIWATA kwa sababu hiyo niliyokusimulia na ujio wa misionari hao wa UMCA. Panapo majaliwa nitamalizia simulizi mbili zilizosalia za Mafuriko ya Chipite na Kifo cha mwandishi Habibu Halahala.
0717649257