…………………………………………………….
Na Rahima Mohamed,Maelezo
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dkt. Hussein Ali Mwinyi imefanya jitihada kubwa ya kujenga miundombinu ya sayansi na teknolojia ili Zanzibar iendane na kasi hiyo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya makaazi Mhe Riziki Pembe Juma kwa niaba ya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Katiba,Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala wakati akizindua chaneli ya Elimu Zanzibar TV (EZTV) huko skuli ya Kwarara Mkoa wa Mjini Magharib ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo inafikia kilele chake kila ifikapo tarehe 12 Januari.
Amesema jitihada za kuimarisha miundombinu ya teknolojia ikiwemo mkonga wa Taifa Nchi nzima ili kuimarisha na kurahisisha mawasiliano kwa lengo la upatikanaji wa elimu nchini.
Aidha Waziri Riziki amewataka Wizara ya Elimu kuhakisha wanakipatia mahitaji yote ya msingi kituo hicho ili kitumike kwa usahihi katika kujifunza na kutoa elimu bora kwa wanafunzi kwa lengo la kukuza mtaala wa elimu nchini.
Vilevile amesema Wizara ya Elimu wanatakiwa waandae mpango madhubuti wa kuhakikisha wanazisaidia skuli zote zilizopo kuwekeza miundombinu ya Tehama ikiwemo tv ili wanafunzi wa skuli hizo waweze kufaidika na televisheni hiyo.
Nae katibu mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Khamis Juma amewataka watendaji wa televisheni hiyo kuwa wabunifu na kukitunza kituo hicho kwa lengo la kutoa huduma bora kwa jamii.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Suleiman Abdallah amewataka viongozi wa wizara hiyo wawasimamie watendaji wa kituo hicho na wanafuata maadili ya utangazaji kwa kuhakikisha amani inadumu nchini.