Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako (Mb) akizungumza wakati akizindua Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania uliofanyika Jijini Dar es Salaam leo Januari 3, 2022.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba, Dkt. Mboni Ruzegea akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania uliofanyika Jijini Dar es Salaam leo Januari 3, 2022.
Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma za Maktaba, Prof. Rwekaza Mkandala akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania uliofanyika Jijini Dar es Salaam leo Januari 3, 2022.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wapya wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania mara baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika Jijini Dar es Salaam leo Januari 3, 2022.
……………………………………………………….
Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Maktaba Mtandao ili kuongeza wigo wa upatikanaji huduma za maktaba kutokana na ongezeko la idadi ya watumiaji wa huduma hiyo nchini.
Hayo yamesemwa leo Januari 3, 2022 Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako (Mb) wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (BOHUMATA) ambapo amesema fedha hizo ni sehemu ya Shilingi bilioni 10.5 za bajeti ya maendeleo ya Bodi hiyo zilizotolewa na Serikali katika mwaka wa fedha 2021/22.
Aidha ameitaka Bodi hiyo kuhakikisha katika utafutaji wa machapisho na vitabu izingatie kupata vitabu vinavyolenga kukuza ujuzi, maarifa na stadi mbalimbali kwa Watanzania wote wakiwemo wenye mahitaji maalum.
“Nitoe rai kwa Bodi kuhakikisha mnatafuta machapisho na vitabu vinavyolenga kukuza ujuzi, maarifa na stadi mbalimbali. Tunataka maktaba iwe kwa Watanzania wote yaani watoto, wajasiriamali, walemavu wa aina mbalimbali, wakulima, wafugaji, watafiti wote waweze kupata huduma hii muhimu,” amesisitiza Waziri Ndalichako.
Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako amewataka wajumbe wa bodi hiyo kupitia Sheria ya Bodi Na. 6 ya mwaka 1975 na kumshauri iwapo inafaa kuendelea kutumika au inahitaji maboresho ili kwendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia nchini na ulimwenguni kwa ujumla.
“Niwape changamoto kuwa Sheria hii ni ya muda mrefu hivyo pamoja na kuitumia kutekeleza majukumu yenu, nategemea kabla Bodi haijamaliza muda wake inipe mapendekezo iwapo sheria hii bado inakidhi au kuna haja ya kuifanyia mapitio ili iendane na teknolojia ya wakati huu,” amesema Prof. Ndalichako.
Akiongea katika uzinduzi huo Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Prof. Rwekaza Mukandala amesema wamepewa dhamana kubwa na Taifa ya kuiongoza Bodi hiyo na kuahidi kutekeleza jukumu hilo kwa umakini, uadilifu na weledi.
Amesema Wajumbe wa Bodi hiyo wanatoka katika nyanja mbalimbali na wana uzoefu wa kutosha na umahiri hivyo anaamini watakuwa na mchango mkubwa utakaoiwezesha Taasisi hiyo kutoa huduma bora na za kisasa kwa wananchi na hivyo kuchangia maendeleo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa BOHUMATA, Dkt. Mboni Ruzegea amesema Bodi hiyo inakusudia kufanya mabadiliko na upangaji upya wa shughuli na huduma za Taasisi hiyo ili kwendana na dira na dhima ya taasisi katika kutekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano 2020/21 – 2024/25.
Amesema Mpango huo unalenga utoaji wa huduma za kisasa za maktaba kwa njia ya kidigitali, utawala na usimamizi wa rasilimali watu na kuimarisha uwezo wa Taasisi katika kutoa huduma kwa wananchi.