Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC),Mkoa wa Dodoma,Ismail Jama,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wakitoa taarifa ya kumpongeza Spika Ndugai kwa kuonesha ukomavu mkubwa kisiasa kwa kitendo chake cha kutoka hadharani na kuomba radhi kwa Mhe. Rais na kwa watanzania kwa jumla.
………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma kimempongeza Spika wa Bunge Job Ndugai kwa kuonesha ukomavu mkubwa kisiasa kwa kitendo chake cha kutoka hadharani na kuomba radhi kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mapema leo Spika Ndugai alizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dodoma na kumuomba radhi Rais Samia ambapo amesema hakuwa na nia mbaya wakati akitoa kauli kuhusu mikopo ya nchi na kwamba kauli yake ilihaririwa na baadhi ya watu wasio na nia njema wenye lengo la kumchonganisha na Rais Samia Suluhu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Januari 3,2022,Jijini Dodoma,Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC),Mkoa wa Dodoma,Ismail Jama amesema Mkoa unampongeza Spika Ndugai kwa kuonesha ukomavu mkubwa kisiasa kwa kitendo chake cha kutoka hadharani na kuomba radhi kwa Mheshimiwa Rais na kwa watanzania kwa jumla.
“Sisi Mkoa wa Dodoma tuko bega kwa began na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumuunga mkono kwa juhudi zake za kusimamia ujenzi wa uchumi wa Taifa letu,”amesema.
Aidha,amempongeza Rais Samia na Mwenyekiti wa CCM,kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya kuwasaidia watanzania kwa kukopa fedha kwa ajili ya maendeleo hususan elimu,afya.
”Wananchi wameona kazi iliyofanyika na inayoendelea kufanyika,kwa mara ya kwanza wanafunzi wa kidato cha Kwanza na Darasa la kwanza wanakwenda shule kwa wakati bila kukosa madarasa na madawati”amesisitiza