*************************************
Adeladius Makwega
Chamwino Ikulu.
Siku ya leo, niliamka saa 12. 15 asubuhi, kwa kuwa nilipanga kusali ibada ya saa 12.00 asubuhi ya Jumapili hii, ili kuanza mwaka na Bwana, muda huo nilioamka nilikuwa nimechelewa lakini nilijiandaa na kuanza safari ya kwenda kanisani kusali Dominika.
Safari hiyo ambayo ni mwendo kama wa dakika kati ya saba na nane kwa mtu ambaye anatembelea kwa hatua kubwa. Nilipita jirani na ukuta wa Ikulu huku kukiwa kumetulia tuli, niliambaambaa na ukuta huo hadi kuelekea Kanisa Katoliki la Chamwino Ikulu ambayo ni Parokia ya Bikira Maria Imakulata, lililopo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.
Ukiwa unatoka usawa wa Ikulu ya Chamwino, kuna njia ya vumbi, niliambaambaa na njia hiyo na nilipokuwa nakaribia kuanza eneo la parokia hiyo, kwa mbele yangu kama mita mia 150 niliwaona wanawake wawili waliokuwa wamevaa kanga na mwingine alikuwa na kilemba cha watawa wa Kanisa Katoliki. Huyu mama wa pili alikuwa anaonekana amejitanda khanga hadi kichwani.
Manawake hawa walienda hadi katika bango linaloitambulisha parokia hii wakawa kama wanasoma muda wa Ibada za parokia hii. Wao wako mbele na mimi naiona miili yao kwa nyuma, nikajisemea mwenyewe, yule atakuwa mtawa kaja kumsalimia ndugu yake, kwa hiyo ndugu yake atakuwa mgeni, au ndugu yake huyo ni mvivu wa kwenda kanisa kwa hiyo hata muda wa ibada hajui? Nilihisi hivyo, ndiyo sababu ya wao kutazama muda. Kwani angekuwa mtawa mwenyeji asingali tazama muda huo katika bango.
Hayo niliyasemea mwenyewe moyoni, waliposoma bango walitoka upande wa bango hilo na kurudi njiani kuelekea kanisani. Kwa kuwa mimi nilikuwa na spidi kali niliwavuka, nilipokuwa nawavuka niliwatazama na kuwasalimia. Nilipowatazama kwa jicho pembe nilibaini kuwa kumbe wote walikuwa watawa wa kike wa Kanisa Katoliki.
Hapo sasa ile dhambi niliyochuma ya kusema kuwa mtawa mmoja kenda kwa ndugu yake mvivu wa kusali nikaomba msamaha wa Mungu wangu. Nikajisemea moyoni pengine hawa watawa wamekuja kuwasalimia watawa wenzao na walikuwa labda wakisoma muda ili wajue wenzao wanatoka saa ngapi kanisani, huko hoja ya ugeni ya watawa hawa wawili ilibaki palepele, nikisema kwanini walisoma bango hilo?
Kilichoendelea kwa watawa wale wawili kama waliingia kanisa au la sikuona, bali nilipoingia kanisa sasa ilikuwa ni wakati wa mageuzi, hapa ndipo wakati wa mkate na dizai zinapogeuzwa kuwa mwili na damu ya Bwana Yesu kwa Imani ya Kikatoliki.
Niliingia kimya kimya mchelewaji mimi na kuketi benchi la mwisho kabisa la kanisa hili upande wa wanaume. Nikiwa kanisani, nilibaini kuwa kanisa hilo ambalo linaonekana kuwa jipya lina mabechi yaliyo katika mistari mitatu na kila mstari una mabechi 15 jumla kulikuwa na mabechi 50 ukijumlisha na mabechi ya waimbaji kwanya. Benchi moja namna lilivyo linaonekana linaweza kukaliwa na watu kati 10-15.
Nilibaini kuwa katika bechi lililokuwa waumini wengi ni lenye watu wanne au watano, mengi yalikuwa tupu.
Kumbuka nimechelewa sana, ukafika wakati wa kupeana Amani ya Bwana, hapo sasa kwa utaratibu wa sasa wa kanisa hakuna kupeana mikono, bali kila mmoja anamgeukia mwenzake na kumuinamia. Hapo nilibaini kuwa wapo ambao walikuwa hawatambua kuwa Korona ilibadilisha hata baadhi ya mambo ya ibada, ikiwamo la kupeana amani kwa mikono. Nilishuhudia jamaa mmoja anatoa mkono na mwenzake anamuinamia tu.
Ibada ilipokuwa inakaribia mwisho, msomaji wa matangazo alienda mbele na kuyasoma matangazo hayo nilikuwa simsikii vizuri kwa kuwa spika hazikufanya kazi yake vizuri, kwa hiyo ilikuwa tabu kidogo lakini alipomaliza aliwaalika viongozi wa jumuiya kama saba za parokia hii mbele ya waamini ili walieleza kanisa michango yao ya zaka kwa mwaka 2021 ilikuwaje? Zaka huwa ni asilimia 10 ya mapato ya kila muamini.
“Jamani mnapaswa kutumia asilimia 90 ya mapato yenu uliyoyatapata lakini asilimia 10 ni kwa ajili yetu hapa kanisani.”
Alisema msomaji wa matangazo.
Kati ya jumuiya saba, jumuiya nne zilivuka malengo yake na pengine zilikuwa na mara mbili ya kile walichopangiwa wakati jumuiya tatu hazikufikia malengo yake.
“Katika makadilio yetu yalikuwa tukusanye milioni 14, kama jumuiya zilivyojieleza mbele yenu zaka zilizokusanywa ni milioni 14 na laki tano, ambapo unatakiwa kutoa ulichokipata katika kazi,biashara, kilimo au mazao yako. Kwa takwimu hizo malengo tumeyavuka.”
Msomaji wa matangazo aliwaomba waamini wa kanisa hilo kujipongeza kwa kuvuka malengo yao.Tulipewa Baraka ya mwisho na kurudi zetu majumbani.
Nilipokuwa narudi nyumbani kwangu nilijiuliza hoja moja kuwa kwanini duniani kumekuwa na desturi ya kuyaangalia mafanikio kwa ujumla wake. Bila ya kujua kuwa kwanini miongoni mwetu hatukufikia malengo tuliyojipangia? Wale wenye mafanikio makubwa wanasababisha wale wanaoshindwa kufikia malengo kujumuishwa kuwa sehemu ya mafanikio ya pamoja.
Nilisema moyoni kuwa ni vizuri katika mafanikio tutazame nakisi kati ya waliofanya vizuri na wale wasiofikia malengo, ili safari ya maendeleo yoyote ile tufike pamoja.Wale waliofanya vizuri ili waweze kuwasaidia wasiofanya vizuri kwa kuelimishana mbinu bora za maisha ya mafanikio. Nakutakia jumapili njema.