***************************
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Vikundi nane vya wanahisa vikoba kutoka katika kata za Ndala na Masekelo Manispaa ya Shinyanga wamesema wameendelea kupiga hatua ya mafanikio kiuchumi kupitia mpango wa vikoba tangu kuanza kwake Mwaka 2012.
Wakizungumza baada ya hafla fupi ya kupongezana na kufanya tathmini ya matokeo ya vikundi hivyo vya hisa wametaja mafanikio mbalimbali waliyofikia tangu kujiunga na mpango huo wa vikoba ikiwemo kujikwamua kiuchumi pamoja na kusomesha watoto shuleni.
Katika lisara yao iliyosomwa na mwenyekiti wa vikundi vya hisa vikoba Ramadhan Kaswa wametaja hatua mbalimbali za mafanikio lakini pia changamoto kadhaa zinazohitaji kutafutiwa ufumbuzi.
“Tumeweza kusomesha watoto wetu na kuwapatia mahitaji muhimu,tumeweza kuwasaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu vilevile wanavikundi wamepata mafanikio ya kubadilisha maisha yao hasa katika kufanikisha upatikanaji wa viwanja na nyuma bora na kuishi katika ufugaji wenye tija”.
“Changamoto tunazopata kwenye vikundi ni baadhi ya wanachama kutokuleta marejesho kwa wakati, inatokana na hali ya kibiasraka kubadilika badilika na pia kutokuwepo kwa ushirikiano wa kifamilia katika matumizi na marejesho ya mikopo”.
Kwa upande wake Afisa maendeleo ya jamii katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Angel Mwaipopo amewataka wanawake waliopiga hatua za mafanikio kuwaibua wanawake wengine hasa waliopo penbezoni ili waweze kunufaika na fursa zilizopo.
Afisa huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo amevitaka vikundi hivyo kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ikiwemo mikopo ya fedha zinazotolewa na Halmashauri ya Manispaa ambapo amesema serikali inaendelea kuwawezesha wanawake kupitia fursa mbalimbal.
Mwaipopo amewata wanavikundi hao kushirikiana, kupendana na kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha ambapo amewasisitiza kuendelea na uaminifu huo ili kuondoa migogoro.
Katika hafla hiyo ilihusisha viongozi mbalimbali wa serikali za mitaa wa kata hiyo wakiwemo wenyeviti wa mitaa na diwani wa kata ya Ndala pamoja na kata ya Masekelo.
Akizungumza diwani wa kata ya Ndala Zamda Shabani amewapongeza wanahisa kwa kuendelea kuwa waaminifu kwenye vikundi vyao ambapo amesema wapo baadhi ya watu huwa na kopa na kushindwa kurejesha na kupelekea migogoro kwa viongozi wa mitaa.
Diwani Zamda amewaomba wanawake kuendelea kuunda vikundi vya kuzalisha ili kunufaika na kutoa ajira kwa wengine.
Naye diwani wa kata ya Masekelo Pitter John amewakumbusha kuwa changamoto zisiwakatishe tamaa ambapo amewasisitiza kuridhika na kile wanachokipata kwenye faida na kwamba wasijiingize kwenye starehe pale wanapopata faida.
Kwa upande wake mwalimu mwezeshaji uchumi wa vikundi hivyo vya hisa vikoba Johari Salum Mmassy amesema wapo watu wanapotoshwa kuwa vikundi vya hisa vina dhulumu watu amesema siyo kweli hivyo amewashauri wanawake na wanaume kujiunga kwenye vikundi vya hisa ambavyo vinawalimu waliosajiliwa na serikali ili kutoka kwenye hatua ya umaskini huku akiwasisitiza akina baba kutoa ushirikiano kwa wake zao hasa kwenye marejesho.
Vikundi vya wanahisa vikoba kutoka katika kata ya Ndala na kata ya Masekelo vimefanya sherehe ya kufunga Mwaka 202, vikundi hivyo vilianza Mwaka 2012 vikiwa vikundi viwili vyenye idadi ya wanachama 30 kwa kila kikundi na sasa wanavyo vikundi 8 vikiwa na wanachama 240 katika kata hizo.