************************
Na John Walter-Babati
Licha ya serikali ya Tanzania kutoa bure huduma za vipimo vya awali vya saratani ya shingo ya kizazi, mwamko wa wanawake wanaopima kipimo hicho ni mdogo.
Saratani ya shingo ya kizazi inaongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi duniani.
Inakadiriwa kuwa asilimia 85 ya vifo hivi hutokea katika nchi zinazoendelea. ambapo Kwa Tanzania, wastani wa wanawake 6,241 huugua saratani hii kila mwaka, ambapo 4,355 kati yao hufa, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la afya duniani (W.H.O) ya mwaka 2010.
Saratani ya shingo ya kizazi ndio saratani ya kwanza kwa wanawake nchini Tanzania, na Saratani namba moja kwa wanawake walio kati ya umri wa miaka 15 hadi 44.
Kwa Afrika Mashariki, asilimia 33.6 ya Wanawake wote, wanasadikiwa kuwa na virusi aina ya human papilloma virus ambavyo ndio visababishi vya ugonjwa huu.
Lakini matumaini yote hayajapotea, saratani hiyo inaweza kuzuiwa na hata kutibiwa ikiwa imegunduliwa mapema.
WHO inapendekeza kwamba wasichana wote wenye umri wa miaka 9-14, kupatiwa dozi mbili za chanjo hiyo kwani njia hiyo inapunguza nafasi ya kuathirika.
Mratibu wa afya ya uzazi Halmashauri ya mji wa Babati Prisca Almasi akizungumza na wanawake na wasichana wa kijiji cha Singu kata ya Sigino katika mpango wa mradi wa Haki ya afya ya uzazi unaofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la Women Fund Tanzania (WFT) na kutekelezwa na Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Manyara amefafanua kuwa wanawake walio kwenye hatari zaidi ni wale wenye wapenzi zaidi ya mmoja kutokana na virusi vinavyosababisha saratani ya shingo ya kizazi kubebwa na wanaume, kundi lingine ni wale walioanza tendo la kujamiana wakiwa na umri mdogo, waliozaa wakiwa na umri mdogo, walioathirika na magonjwa ya ngono, Watu wenye kinga hafifu ya mwili au magojwa kama Ukimwi, wanaozaa mara kwa mara,Wanawake wanaovuta Sigara,wenye wapenzi wengi, uzito mkubwa na kutofanya mazoezi na dalili zake zinaweza kujionyesha kuanzia miaka 10 hadi 15.
Almasi amesema kwa kuwa saratani ya mlango wa kizazi ni hatari na miongoni mwa ugonjwa ambao unaondoa maisha ya wanawake wengi hapa nchini ni vyema wanawake wakajijengea utaratibu wa kufanya vipimo ambavyo ni bure katika hatua za mwanzo na kudai idadi kubwa wanaojitokeza kufanya kipimo hiko wanakuwa tayari wameshaathirika.
Pia ameshauri wakati wa kujisafisha sehemu za siri, wanawake wasitumie sabuni kujisafisha ndani kwa kuwa zinakemikali ambazo zinaua bakteria wa asili wanaolinda maeneo ya uke.
Na iwapo msichana atakua ashaathirika na ugonjwa wa saratani tayari basi hafai kudungwa chanjo hiyo.
Mratibu wa mradi huo Jaliwason Jasson alisema jitihada zaidi zinahitajika katika utoaji elimu na uhamasishaji wanawake kujitokeza kupima kama inavyosisitiza serikali.
Aidha amehimiza utolewaji wa elimu zaidi juu ya ugonjwa huo hasa kwa wanawake waishio vijijini ambao huhitaji taarifa zaidi za afya, hasa hii ya saratani ya shingo ya kizazi ambayo ni miongoni mwa magonjwa yanayo waathiri wanawake walio wengi.
Klabu ya waandishi wa Habari mkoa wa Manyara (MRPC) kupitia mradi wake wa Haki ya Uzazi kwa Wanawake na Wasichana kwa ufadhili wa WOMEN FUND TANZANIA imekuwa ikisaidia programu mbalimbali za kutoa elimu kwa makundi hayo kuzingatia njia sahihi za uzazi wa mpango na kuepuka tabia hatarishi zitakazosababisha maradhi mbalimbali ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi.