……………………………………………………..
Adeladius Makwega,Dodoma.
Wawanji ni kabila mojawapo ambalo lipo katika Mkoa wa Njombe ambalo lina makaazi yake katika safu ya milima ya Livingstone ambayo ina ardhi yenye rutuba nyingi. Kabila hili linaaminika kuwa limegawanyika katika makundi kadhaa; Kundi la kwanza ni Wawanje asilia ambao ni wakaazi wa maeneo ya Matamba, Magoye na Mlondwe.
Lakini pia kuwa Wavilama, hawa wanapatikanana katika maeneo ya Ikuro wakitafautiana na Wawanji asilia kwa matamshi ya baadhi ya maneno ya lugha yao, pia wakitenganishwa mipaka ya kijiografia hasa hasa Mto Nhumbe.
Kabila hili linapakana kwa Kaskazini na Wasangu, Mashariki wakipakana na Wabena, Kusini wakipakana na Wakinga, Kusini Magharibi wakipakana na Wanyakyusa na Magharibi wakipakana na Wasafwa.
Inaaminika kuwa kabila la Wawanji wana asili ya makabila ya Wabena, Wakinga na Wanyakyusa kwa sababu moja kubwa ya majina yao ya ukoo yanalingana fika na majina ya makabila hayo niliyokutajia.
Kwa kuutazama utani katika kabila la Wawanji inaaminika unafanyika baina ya wao kwa wao mathalani babu na mjukuu, bibi na mjukumu kaka na binamu yake. Ambapo inaaminika kuwa binamu anaweza kuolewa na kaka yake binamu na hata kama binamu wa kike atafiwa na mumewe binamu wa kiume anaweza kukaa na binamu huyu wa kike na kumuoa kama mke wa pili.
Hapa pia hata mume wa dada anaweza kumuoa mdogo wa mkewe wa kike na kuishi naye bila tabu yoyote ile kwani kwa utamaduni wa Wawanji mahusiano haya hayana kipingamizi.
Wawanji wanafanya utani baina ya marafiki wa karibu mathalani mke wa rafiki yako unaweza kumtania katika mambo kadhaa ikiwamo hata kukupatia chakula na pombe kwa uhuru kabisa, lakini hakuna utani katika mahusiano ya kimapenzi na shemeji yako(kati ya rafiki na rafiki). Wawanji wenyewe utani huu huwa wanautambua kama “Mulamuvange”.
Jambo ambalo linashangaza wengi ni moja tu kwa kabila hili, kwamba halina utani na makabila mengine japokuwa inafahamika kuwa kwa kuwa Wawanji wengi wanalinganishwa na Wakinga, Wabena na Wanyakyusa. Basi hapo Wangoni wanapenda kuuvunja mwiko wa Wawanji, mara nyingi wanawatania Wawanji wakidhani kuwa ni miongoni mwa watu wanaotokana na makabila haya matatu hasa kutokana na majina yao. Hata Wangoni wakiambiwa huwa wao ni Wawanji hawakubaliani na hoja hiyo wao uendeleza utani.
Lakini kiukweli Wawanji huwa hawana utani na kabila lolote lile lakini Mgoni anaweza kufika kwa Mwanji akafanya vurugu zake naye Mwanji akakaa kimya tu akitambua kuwa Mgoni huyo anafanya hivyo vituko vyake makusudi kwa hoja ya kudhani ndugu huyo ni Mbena, Mkinga au Mnyakyusa.
Swali la kujiuliza ni moja tu je kwanini Wawanji hawana utani na kabila lolote? Jibu lake ni kuwa Wawanji hawakuwahi kupigana vita na kabila lolote lile kwa kuwa, kwanza ni kabila la watu wachache mno, hadi mwaka 1975 ilikadiliwa kuwa Wilaya ya Njombe wakati huo ikiwa sehemu ya Mkoa wa Iringa ilikuwa na Wawanji 24,797 tu. Kwa upande dhana za kivita silaha zao ni za kawaida hasa kwa ajili ya kuwindia tu si kwa ajili ya kupigania vitani na adui aliye mbali, zikiwa silaha zenye mipini mifupi mifupi.
Kwa hakika jamii kadhaa huwa zina mbinu za kujilinda, kwa jamii ambazo ni dhaifu mara nyingi ujenga utaratibu wa kuogopwa kwa kuwa washirikiana sana na jambo hilo huwa ni ulinzi mkubwa kwao. Hilo ndivyo ilivyo kwa Wawanji.
Ikiaminika kuwa kila kabila ambalo lilikuwa linataka kupigana na Wawanji walikuwa wapole, wakiogopwa kufanyiwa ulozi. Wawanji walikuwa makini wakijua tu mnakuja kuwavamia waliweza kuwatuma vijana wao na kuja hadi katika ngome ya adui na kuchota michanga yenye nyayo (hatua) za hao askari na kukimbia na mchanga huo kwa nguvu za giza.
Mchanga huo ukishachotwa ulipelekwa kwa mganga na yeye huufanyia uchawi na kisha wale maadui waliokuwa wakipanga kuwavamia walipotea njia na kuzunguka na kupotezana na kushindwa kufanya vita na kurudi walipotoka.
Kitendo cha ulozi huo kilifahamika kama “Kifughala”. Kuna wakati maadui hao walikuwa wakipotea na baadaye maadui wakigundua wamefanyia ulozi walikasirika pale walipoaguliwa ulozi huo, waliwasaka Wawanji na wakati huo wanakuwa wamekimbia makaazi yao na maadui walichukua vyakula na kuchoma moto makaazi ya Wawanji.
Angalia namna Wawanji walivyogundua kuwa hawana nguvu waliwekeza akili zao katika ulozi. Mwanakwetu ukishatambua madhaifu yako hakikisha uwe na silaha yako moja ya ushindi ya kumuangamiza adui kama walivyo Wawanji na ulozi wao. Nakutakia mwaka mpya mwema wa 2022.
0717649257.