****************************
Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Julai 2018, Waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi na ajira alisitisha huduma ya kuunganisha Watanzania na fursa za ajira nje ya nchi kupitia Mawakala Binafsi wa Huduma za Ajira. Hatua hii ilitokana na ukiukwaji mkubwa wa sheria na kanuni uliokuwa ukifanywa na baadhi ya Mawakala. Vilevile, Serikali ilichukua hatua hizo ili kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha Watanzania kunufaika zaidi na fursa za ajira nje ya nchi.
Serikali inatambua umuhimu wa kuwezesha Watanzania kunufaika na fursa za ajira za staha nje ya nchi zinazojitokeza kutokana na: ushiriki wa Tanzania katika Jumuiya za Kikanda; mahusiano ya kihistoria kati ya Tanzania na baadhi ya nchi duniani; pamoja na ushiriki wenye tija wa nchi yetu kwenye Jumuiya/Mashirika/Taasisi na Asasi za Kimataifa.
Aidha, Serikali inatambua na kuzingatia kuwa katika kutumia fursa za ajira nje ya nchi usalama na haki za msingi kwa Watanzania ni suala lisilo na mbadala na hivyo ni lazima uunganishaji wa watanzania na fursa za ajira nje ya nchi uzingatie viwango vya kazi za staha vinavyokubalika na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Kwa sasa, fursa nyingi za ajira nje ya nchi zinajitokeza kutokana na sababu zifuatazo:-
- Kupiga hatua kwa mitangamano ya kikanda (advancing regional integrations) kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki inayotekeleza Itifaki ya Soko la Pamoja, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU) ambapo uhamaji huru wa nguvukazi unaendelea kuwa agenda muhimu. Kukua kwa mashirikiano kunaenda sambamba na uptikanaji wa fursa mbalimbali zikiwemo fursa za ajira kwa watanzania wenye sifa stahiki;
- Uanachama na ushiriki wenye tija wa nchi yetu kwenye Jumuiya/Mashirika/Taasisi na Asasi za Kimataifa ambapo suala la uhamaji huru wa nguvukazi ni moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele na Jumuiya za Kimataifa;
- Mashirikiano ya kibiashara baina ya nchi yetu na mataifa mengine (bilateral trade agreements) ambayo kwa kawaida huenda sambamba na uhamaji wa mitaji pamoja na nguvukazi;
- Mahusiano ya kihistoria kati ya Tanzania na baadhi ya mataifa. Tanzania ina mahusiano ya kihistoria na ya muda mrefu na baadhi ya mataifa jambo ambalo limekuwa kichocheo cha uhamaji wa nguvukazi kutoka Tanzania kwenda kwenye mataifa husika;
- Kusaini Mkataba (bilateral agreement) na nchi ya Qatar unaoweka uratibu na usimamizi wa fursa za ajira kwa Watanzania nchini Qatar pamoja na kuanza mazungumzo na baadhi ya mataifa ya kimkakati.
Kwa kutambua mchango mkubwa wa fursa za ajira zinazopatikana nje ya nchi katika maendeleo ya nchi yetu, na kwa kuzingatia kuwa, tunao Mwongozo kwa Mawakala Binafsi unaobainisha masuala ya msingi katika kuunganisha watanzania na fursa za ajira nje ya nchi, tunapenda kuufahamisha umma wa Watanzania hususani Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira pamoja na Watanzania wenye shauku na sifa ya kufanya kazi nje ya nchi kuwa, shughuli za kuunganisha Watanzania na fursa za ajira nje ya nchi kupitia Mawakala Binafsi wa Huduma za Ajira zinarejeshwa rasmi kuanzia leo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni pamoja na Mwongozo Mpya.
Hivyo basi, tunawajulisha Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira nchini ambao wamepata fursa za ajira kwa Watanzania nje ya nchi kuwasilisha maombi yao kwa Mkurugenzi wa Huduma za Ajira (TaESA), S.L.P. 80384, Barabara ya Bibi Titi Mohamed, Dar es Salaam ili waweze kupatiwa vibali vya kuunganisha watanzania na fursa husika. Pamoja na mambo mengine, maombi ya kuunganisha watanzania na fursa za ajira nje ya nchi yatakayoshughulikiwa hayanabudi kukidhi vigezo muhimu vifuatavyo:-
- Wakala husika kuwa na leseni ya kuunganisha watanzania nje ya nchi inayotolewa na Kamishna wa Kazi. Kwa wale wasio na leseni na wana fursa za ajira nje ya nchi wawasilishe maombi ya leseni kwa Kamishna wa Kazi iliyopo jengo la NSSF Mkoa wa Dodoma, Barabara ya Mwangosi/ Posta, S.L.P 2890, Dodoma yakiambatana na ada ya usajili ya kipindi cha mwaka mmoja isiyorudishwa kiasi cha Tshs 500,000 (Laki Tano tu). Vigezo vinavyotumika kuwapatia leseni Mawakala kuunganisha watanzania na fursa za ajira nje ya nchi vinapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu (pmo.go.tz) na (www.kazi.go.tz);
- Fursa za ajira ziwe ni zile za kuunganisha Watanzania wenye ujuzi na kazi husika (ujuzi wa chini, kati na juu) wenye kiwango cha elimu kuanzia sekondari na kuendelea au wenye cheti cha mafunzo ya ujuzi ya muda maalum yanayohusiana na kazi husika kutoka chuo kinachotambulika na serikali;
- Wakala kutumia kanzidata ya Watafutakazi iliyopo Kitengo cha Huduma za Ajira (TaESA) kuwapata/kuchuja watanzania wenye sifa kwa kazi husika. Wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo wanasisitizwa kuendelea kujiandikisha kwenye kanzidata ya Watafutakazi ya serikali;
- Mikataba ya ajira kuzingatia viwango vya kazi vilivyowekwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO);
- Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira kuhitajika kuweka kiwango maalumu cha fedha (security bond) kwenye ubalozi wa Tanzania kwenye nchi anayounganisha watanzania ili kuwezesha kuwarejesha Wafanyakazi wa Tanzania wanaopata changamoto za msingi na kulazimika kurejea nchini kabla ya mkataba kuisha;
- Kwa usimamizi wa TaESA, Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira kuwezesha kutoa mafunzo maalum ya kujenga uzalendo, mazingira ya kazi pamoja na tamaduni za nchi husika kwa Watanzania wote watakaokuwa wamekidhi vigezo kabla ya kusafiri kwenda kwenye nchi husika;
- Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira husika kutoa taarifa kila robo mwaka idadi na hali ya watanzania waliounganishwa kufanya kazi nje ya nchi;
- Pamoja na vigezo vingine muhimu vilivyobainishwa kwenye Mwongozo.
Mwisho tunatoa wito kwa Wadau wote kuzingatia mambo muhimu kama ifuatavyo:-
- Ni kinyume cha Sheria kufanya kazi ya kuunganisha watanzania na kazi nje ya nchi bila kuwa na leseni halali iliyotolewa kwa mujibu wa Sheria;
- Watanzania wote wenye sifa na shauku ya kufanya kazi nje ya nchi wanahimizwa kufuata utaratibu rasmi wa kwenda kufanya kazi nje ya nchi. Kila Wakati, Serikali itakuwa inaweka hadharani orodha ya Mawakala Wanaoruhusiwa kuunganisha Watanzania nje ya nchi;
- Kwa Mawakala Binafsi wa Huduma za Ajira, au Watu Binafsi wanaojihusisha na kuunganisha Watanzania na fursa za ajira nje ya nchi kinyume na sheria na taratibu za nchi, Tunawataka kuacha Mara Moja kujihusisha na huduma hizi;
- Maelezo zaidi kuhusu taratibu za kuunganisha watanzania na fursa za ajira nje ya nchi yanapatikana Ofisi za Kitengo cha Huduma za Ajira (TaESA) zilizopo Arusha, Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza.