Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akikabidhi hundi ya fedha kwa kikundi cha wajasiliamali wa Sumbawanga leo.
Picha ya pamoja viongozi wa Mkoa wa Rukwa wa Chama na Serikali Leo wakati wa hafla ya utoaji mikopo yenye thamani ya shilingi Milioni 118 Kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu iliyotolewa na Manispaa ya Sumbawanga leo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (aliyevaa tai) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba (kulia) Leo wakati wa hafla ya utoaji mikopo kwa vijana, wanawake na walemavu ikiwa ni mapato ya ndani ya Halmashauri kukuza uchumi.
( Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa).
************************
Vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wametakiwa kutumia mikopo ya fedha Vifaa walivyopatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kukuza uchumi wa kaya na kuzalisha ajira miongoni mwa wanufaika.
Hayo yamebainishwa leo (31.12.2021) na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti wakati wa hafla ya kukabidhi mikopo ya bajaji, bodaboda na fedha kwa wajasiliamali iliyofanyika katika viwanja vya bustani ya Mandela mjini Sumbawanga.
” Ni vizuri mkatumie fedha hizi kwa lengo la kukuza ajira na kipato cha kaya zenu na Taifa kwani serikali inatoa fedha hizi kama mkopo na mtakaporejesha basi vijana na akina mama wengine watanufaika nayo” alisisitiza Mkirikiti
Aidha amewapongeza wanufaika kwa kurejesha mikopo yao yote ya awamu ya kwanza bila usumbufu na ameagiza kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoa elimu zaidi ili wananchi wajue namna ya kupata mikopo na kuweza kujikimu.
Katika hafla ya leo Manispaa ya Sumbawanga imetoa mikopo isiyo na riba yenye jumla ya shilingi Milioni 118.5 .
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Sumbawanga Frank Mateni amesema mikopo hiyo ambayo jumla yake inafikia shilingi Milioni 118.5 imetolewa ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2020-2025) pamoja na bajeti ya serikali na mkakati wa kuwezesha wananchi kiuchumi kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri.