Mbunge wa Jimbo la Mwera Zahour Mohamed Haji akimtwisha ndoo ya maji mmoja wa wananchi wa Mtoni katika uzinduzi wa maji safi na salama uliofanyika Mtoni kidatu matopeni Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja.
Mbunge wa Jimbo la Mwera Zahour Mohamed Haji akinywa maji kuashiria uzinduzi maji safi na salama katika Jimbo lake la Mwera uzinduzi huo umefanyika Mtoni kidatu matopeni.
Mbunge wa Jimbo la Mwera Zahour Mohamed Haji akizungumza na wananchi wa Mtoni kidatu matopeni kwenye hafla ya uzinduzi wa maji safi uliofanyika Mtoni kidatu matopeni.
Fundi wa visima vya maji Hafidh Khamis Hafidh akimpa maelezo Mbunge wa Jimbo la Mwera Zahour Mohamed Haji juu ya namna wanavyofanya mgao wa maji kwa wananchi wa Mtoni kidatu matopeni.
Picha na Makame Mshenga.
************************
Na Khadija Khamis – Maelezo .Zanzibar .31/12/2021
Mbunge wa Jimbo la Mwera Mhe. Zahour Mohamed Haji amewataka wananchi kuhifadhi na kulinda miundombinu ya maji, ili idumu kwa muda mrefu na kusaidia jamii.
Kauli hiyo ameitoa huko Mtoni Kidatu Chemchem Wilaya ya Magharibi ‘’A’’ wakati wa Uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama mara baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa.
Aidha alisema mashirikiano yanahitajika katika kuitunza miundombinu hiyo ili lengo la Serikali kuwaondoshea usumbufu wananchi wake liweze kufanikiwa.
Alifahamisha lengo la kuzindua mradi huo ni kuwasaidia wananchi wa huko hasa akinamama ambao walikuwa na kilio cha muda mrefu pia ni miongoni mwa ahadi alizoahidi kuzitekeleza .
Alisema ataendelea kutoa huduma mbali mbali za kijamii ambazo zimekuwa ni changamoto kubwa ikiwemo utengenezaji wa miundombinu ya barabara kuwapatia mtaji, mafunzo pamoja na masoko wajasiriamali wadogo wadogo ili kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao.
Aidha alisema katika jitihada za kutatua changamoto zilizopo ni pamoja na kuongeza mashine za kusukumia maji ili zirahisishe kusambaza maji kwa haraka na kuahidi kutoa sh. 340,000 kwa kila mwenzi kwa ajili ya gharama za umeme.
Hata hivyo aliitaka kamati ya kusimamia maji na kufanya matengenezo kila panapoharibika ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
“Serikali haitaki ubaguzi hivyo ni marufuku kujitokeza mtu kujimilikisha mradi huo “alisema Mbunge Zahour.
Nae Katibu wa kamati ya mradi wa kisima hicho Mwalimu Mohamed Ali Juma alimpongeza Mbunge huyo kwa kuwapatia huduma hiyo ambayo walioikosa kwa muda wa miaka sita.
Alisema ameahidi kushirikiana na wanakamati wenzake ili kuhakikisha huduma hiyo inadumu na kuwasaidia wananchi wa mwera Hadi mtoni kidatu .
Kwa upande wake Bi Asha Mohamed Khatibu kutoka shehia ya mtoni kidatu Chemchem ametoa shukrani kwa Mbunge huyo kwa niaba ya wanawake wenzake kwa kuwatuwa ndoo kichwani na kuwaondoshea usumbufu wa ukosefu wa huduma hiyo.
Akitoa wito kwa wanajamii alisema
Kutoa mashirikiano kwa kuchangia mambo madogo madogo yanapohitajika ili tukiwezeshe kisima hicho kiwe endelevu kitusaidie na vizazi vijavyo.