……………………………………………….
Adeladius Makwega
Dodoma.
Wayao ni kabila linalochukua ukoo kwa baba na wanapatikana Kusini mwa Tanzania, Kasikazini mwa Msumbiji na huku wengine wakiishi sehemu za Malawi. Wayao wanaoishi Tanzania hasahasa wanapatikana katika wilaya kubwa mbili nazo ni Masasi na Tunduru. Kwa sehemu kubwa Tunduru ni kwa Wayao lakini Masasi ina Wayao na Wamakua.
Wayao na Wamakua wamekuwa na ujirani mkubwa huku yakioleana tangu enzi. Wayao kwa sehemu kubwa wamezungukwa na Wamakonde kwa upande wa mashariki huku kwa upande wa magharibi wakipakana na Wangoni na Kaskazini wakipakana na Wamwera.
Kwa desturi Wayao ni wakulima wa mazao mbalimbali ikiwamo Korosho, Karanga, Vitunguu, Mtama, Mahindi, Mihogo, Viazi Vitamu na Maharage huku likiwa kabila lisilo na desturi ya kufuga wanyama wowote wale.
Suala la Wayao kutokufuga kunatokana na sababu kubwa mbili kwanza wamekuwa ni kabila lililokuwa likipambana na vita kila mara na makabila yanayolizunguka hasa kwa upande wa Kusini wa Tanzania. Pili hata kama walikuwa na makaazi ya kudumu wali sumbuliwa na wadudu ambao walikuwa na madhara kwa mifugo hiyo.
Wayao ambao leo wapo Tanzania walitokea Msumbiji katika makundi makubwa mawili, kundi la kwanza walivuka kupitia Mto Ruvuma na kundi la pili lilikuja kwa kupitia Malawi. Wayao waliopitia Malawi walibainia kuwa eneo hilo ambalo lilikuwa na rutuba na maji ya kutosha lilikuwa zuri kwa kilimo tayari kulikuwa na makabila mengine ambayo yalikuwa na nguvu za kivita yalishaweka kambi, wakiwamo Wangoni na Wanyasa.
Wangoni kwa kuwa walikuwa mafundi wa vita waliwashinda Wayao na kuwafurusha Mashariki ya Malawi na ndipo wakaibukia Masasi. Walipofika Masasi walikutana na ndugu zao Wayao wengine walishafika Masasi ambao ndiyo wale waliovuka kupitia Mto Ruvuma kwa hiyo wakaweka kambi hapo.
Vita hivyo ambavyo Wayao walipigana na Wangoni wakiwa Malawi vilipewa jina “Ngondo ja Makwangwala” ikimaanisha vita vya ukombozi wa Makwangala-Vita vya Ukombozi na watu wasiokwenda jandoni.
Kwa desturi Wayao walikuwa ni kabla lenye asili ya kupeleka jandoni vijana wao tangu enzi, jambo hilo liliwafanya kujiona wao kuwa ni zaidi ya kabila lolote lile. Swali ambalo mimi binafsi nilijiuliza ilikuwaje Wayao wakawapachika Wangoni jina hilo la Makwangala? Je, Wayao walijuaje kuwa Wangoni ni Makwangala? Je Wayao waliwatuma mabinti zao wakawachunguze watani wao Wangoni au vilikuwa ni vijembe na fitna vya Wayao kwa Wangoni? Maswali hayo nitayatafutia majibu yake siku nyengine.
Utani kwa kabila la Wayao huanza tangu mtoto anapozaliwa kwani hupatiwa jina la muda ambapo jina hilo huwa ni jina la mababu waliotangulia, jina hilo kwa Kiyao linaitwa “Lina lya Uvile.” Jina analopewa mtoto kwa utani. Inawezekana mtoto akapewa jina la mtu ambaye alikuwa mchawi, mvivu na hata mwizi lakini akiwa mtoto wa kiume jina hilo akienda jandoni jina la somo linakufa anapata jina jipya. Hapo hakuna mwenye kibali cha kuliita jina hilo tena labda wale walienda jandoni pamoja tu ambao vijana hao hufahamika kama “Chikudi”.
Kwa sehemu kubwa Wayao wana utani na makabila mengi lakini kabila pekee ambalo lina utani mkubwa na Wayao ni Wamwera ambao wapo katika Wilaya ya Nachingwea na Lindi. Wamwera wanazungumza lugha inayofahamika kama Kimwera. Nakumbuka Nikiwa mwanafunzi wa Ndanda miaka ya 1990 nilibaini kuwa Lugha ya Kiyao na Kimwera zinafanana sana na mimi binafsi nilishindwa kuzitafautisha.
Ikiaminika kuwa Wayao na Wamwera wenyewe wanatambuana, Mmwera akizungumza na Myao na Myao akizungumza na Mwera huwa kama kila mmoja anataka kuzungumza lugha ya mwenzake lakini anaikosea. Niliambiwa kuwa hapo sasa kila mmoja humcheka mwenzake.
“Huyo anataka kuzungumza Kiyao hakiwezi na huyo anataka kuzungumza Kimwera hakiwezi.”
Hapo sasa ndipo utani wa makabila haya uliibuka. Hapo kila mmoja akielewa kila kitu kinachozungumzwa na mwenzake na kujibu kila kitu.Tofauti ni katika kuyatamka baadhi ya maneno huku misamiati ikiwa ni ile ile.
Utani pia unaonekana pale Myao anapofiwa, Wamwera huwa ndiyo wenye jukumu la kuchimba kaburi na kuzika huku Wamwera wanawake wao huwa na jukumu la kuchota maji, kupika hadi msiba ukimalizika, hilo huwa hata kwa Mmwera akifariki Wayao huwa na majukumu hayo hayo.
Wayao na Wamwera pia huwa wanautani katika pombe ambapo pombe inatengenezwa vizuri labda huyo ametengeneza ni Myao, hapo Mmwera anaweza kwenda na kundi la Wamwera wenzake wakaingia ndani ya nyumba wakautoa mtungi wakanywa alafu wakaondoka zao, hapo hakuna kushitaki popote kama umechukia ngoja nao Wamwera watengeneza pombe yao nenda kalipize kisasi. Pombe hiyo kwa Kiyao inaitwa “Nkologo wa Uvile.”
Jambo kubwa na la kushangaza Wayao na Wamwera huwa hawana utani baina ya mwanamke na mwanamme, utani uliopo ni kwa mwanamke na mwanamke au mwanaume na mwanaume tu.
Wayao pia wanautani na makabila mengine kama vile Wamakonde, Wamakonde kwa desturi na mabingwa wa kucheza ngoma ya Sindimba kwa hiyo Wayao wamekuwa hata na desturi ya kuwaalika Wamakonde kwenda kutoa burudani ya ngoma hiyo katika sherehe za Wayao.
Mialiko hiyo imeleta utani hata kila Myao anapokutana na Mmakonde hutaniana. Kwa mfano kuna wakati alikutana Myao na Mmakonde katika sherehe za Krisimasi Myao akamwambia Mmakonde, ehe naleta ngoma hapa uje utuchezee tuburidike. Utuchezee hata kwa dakika 10 hivi. Mmakonde kwa kebehi akajibu kuwa sawa nitafanya hivyo lakini akikisha mama zako wote na dada zako wote wawepo na hapo ndipo na mimi nitacheza ngoma hiyo. Mwisho wa siku kila mmoja anacheka maisha yanaendelea.
Utani mwingine wa Wayao na Wamakonde upo katika kunywa pombe, Wamakonde mara nyingi katika msimu wa kiangazi huwa wanafunga safari hadi kwa Wayao kwenda kunywa pombe. Wayao wanaaminika ni mabingwa wa kutengeneza pombe. Wamakonde wakifika huko huwa wanalewa kwa haraka mno pombe hiyo.
Kwa hiyo Wayao kama wakiwa na mtu ambaye akinywa pombe kidogo analewa mtu huyo hutafanishwa na Mmakonde.
“Valandite kung’wa Chimakonde.”
Kwamba anakunywa pombe kama Mmakonde.
0717649257